Sunday, 9 October 2016

Kifimbo cha Malkia kutua Bongo Aprili 8 maandalizi ya kukipokea kuanza mwezi ujao jijini Dar



Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete na Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi wakiwa na Kifimbo cha Malkia wakati kilipotua Ikulu jijini Dar es Salaam mwaka juzi.
Na Mwandishi Wetu
KIFIMBO cha Malkia wa Uingereza kinatarajia kuwasili nchini Aprili 8 mwakani ikiwa ni maandalizi ya Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Gold Coast, Australia 2018 kuanzia Aprili 4 hadi 15.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazopitiwa na mbio hizo za kifimbo cha Malkia, ambacho hupokewa na mkuu wa nchi.

Bayi alisema kuwa maandalizi ya kupokea kifimbo hicho yataanza mwezi ujao wakati TOC itakapokutana na wadau mbalimbali ili kuteua kamati maalum ya itakayoratibu ujio wa kifimbo hicho.

Aliwataja baadhi ya wadau hao kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa mkoa, ofisi ya Mambo ya Nje na wengine wengi.

Alisema kuwa wanasaka wadhamini ili kufanikisha ujio wa kifimbo hicho, ambapo zinahitajika zaidi ya sh milioni 60 wakati wenyeji Australia wameipatia TOC kiasi cha dola z Marekani 3,000 tu, ambazo ni sawa na sh. Milioni 6.

Bayi alisema kuwa wadhamini hao wanatarajia kuwa ubalozi wa Uingereza, Kampuni ya vinywaji ya Peps Cola ambayo mara ya mwisho kilipokuja kifimbo hicho walisaidia sana, Acacia na ITV, Azam TV na vyombo vingine vya habari.

Alisema kuwa wadhamini wakubwa ni pamoja na British Council, Ubalozi wa Uingereza, Peps na Shirika la Kimataifa la Watoto Duniani, Unicef.

Mwaka 2014 Kifimbo cha Malkia kilitua nchini na kukimbizwa katika barabara mbalimbali za jijini Dar es Salaam kabla ya kutua Ikulu, ambako kilipokewa na Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Mrisho Kikwete na baadae kuzungumza na wana michezo.

Kifimbo hicho kilikuwa maalum kwa ajili ya Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Glasgow, Scoland


Michezo hiyo itafanyikia katika jiji la Gold Coast City, lililopo kusini ya Jimbo la Australia la Queensland, ambapo hii itakuwa ni mara ya tano kwa Australia kuandaa, ambapo pia iliwahi kuandaa mwaka 1938 Sydney, 1962 Perth, 1982 Brisbane na mwaka 2006 Melbourne.





Friday, 7 October 2016

Ukata waisumbua timu ya taifa ya Nigeria `Super Eagles'



ABUJA, Nigeria
TIMU ya taifa ya Nigeria itachelewa kufika katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Zambia baada ya kuahirisha kuondoka kutokana na matatizo ya fedha.

Timu hiyo sasa itabidi kuwasili saa 22 tu kabla ya mchezo wake huo uliopangwa kupigwa Jumapili nchini Zambia katika mbio za kusaka kufuzu kwa fainali zitakazofanyika Urusi.

Wachezaji wa timu hiyo badala ya kuondoka mapema sasa walitarajia kuondoka leo kwenda Zambia.

Kwa ratiba hiyo kikosi cha timu hiyo sasa kinatarajia kutua leo mchana, na kinatarajia kufanya mazoezi mara moja tu kabla ya kuikabili Zambia kesho Jumapili.

Amaju Pinnick, kiongozi wa Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF), aliiambia kamati ya michezo ya Bunge kuwa NFF inakabiliwa na ukata wa kulipia ndege ya kukodi na malazi.

Kiongozi wa NFF pia alithibitishi kuwa wachezaji wanaocheza soka Ulaya wametakiwa kujilipia tiketi zao za ndege na kutumia daraja la kawaida ili kujiunga na kambi ya timu hiyo katika mji mkuu wa Nigeriua, Abuja.

Mwezi uliopita, timu ya taifa ya Olimpiki ya Nigeria iliwasili saa chache kabla ya mechi yao ya kwanza kutokana na matatizo ya usafiri.

Neymar afunga Brazil ikiiadhibu Bolivia kwa mabao 5-0 mbio za kwenda Urusi 2018


Neymar wa Brazil (kulia) akichuana na mchezaji wa Bolivia, Yasmani Duk wakati wa mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia Urusi 2018 uliofanyika jana Natal, Brazil. Wenyeji walishinda mabao 5-0.

BRASILIA, Brazil
MCHEZAJI nyota Neymar alifunga bao moja na kutengeneza mengine mawili zaidi wakati Brazil ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Bolivia katika mbio za Amerika ya Kusini za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018.

Neymar, ambaye ni nyota wa Barcelona alifunga bao la 49 katika mechi ya kimataifa ikiwa ni mara yake ya 73 kuichezea Brazil na kumzidi Zico katika ufungaji wa mabao mengi wa wakati wote. 

Akiwa bado na umri wa miaka 24 tu, Neymar anaweza kufikia rekodi ya Pele ya kufunga mabao 77 kutoka katika mechi 91 huku akiwa bado namechi kadhaa kabla ya kufikia 91.

Ushindi huo wa Brazil umeiacha timu hiyo ikiwa katika nafasi nzuri ya kutwaa nafasi ya kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi. 

Timu hiyo sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi tisa. 

Pia huo ni ushindi wa tatu mfululizo kutoka katika mechi tatu kwa kocha Tite, aliyeteuliwa baada ya kutimuliwa kwa Dunga Juni. 

Mbali na Neymar, wachezaji wengine walioingarisha Brazil kwa mabao ni pamoja na Philippe Coutinho, Filipe Luis na  Gabriel Jesus na kuiwezesha timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 4-0 hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Mchezaji mwenzake Coutinho katika Liverpool, Roberto Firmino alifanya matokeo kuwa mbele kwa 5-0 kwa bao la kichwa lililofungwa katika dakika ya 75.

Neymar aliifungia Brazil bao la kuongoza katika dakika ya 10 tu.  Brazil sasa itasafiri hadi Venezuela kucheza Jumanne dhidi ya timu hiyo ambayo haijashinda hata mchezo mmoja.