Saturday, 7 May 2016

Bayern Munich yatwaa taji la nne mfululizo Ujerumani baada ya kuifunga Ingolstadt 2-1



MUNICH, Ujerumani
BAYERN Munich leo wametwaa ubingwa wa Bundesliga kwa mara ya 26 huku ukiwa umebaki mchezo mmoja kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya nchi hiyo huku mabao mawili ya Robert Lewandowski yaliiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ingolstadt.

Kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kimejifariji kwa ushindi huo baada ya juzi kutolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya katika nusu fainali kwa kutwaa kwa mara ya nne mfululizo taji hilo la Ujerumani la Bundesliga.

Lewandowski aliiweka mbele Bayern kwa bao la penalty kabla hajaongeza bao jingine kwatimu hiy kufuatia pasi ya Xabi Alonso.

Penalti ya Moritz Hartmanni ilifanya matokeo hayo kuwa 2-1 lakini imefanikiwa kutetea taji lake hiyo.

Kutawala Nyumbani
Borussia Dortmund ndio timu pekee inayoweza kukishika kikosi cha kocha Guardiola lakini kufungwa kwake bao 1-0 na Eintracht Frankfurt kuna maana kuwa Bayern Munich iko mbele kwa point inane mbele ya mpinzani wake mkubwa wakati akicheza mechi za wikiendi hii.

Guardiola ataanza kibarua chake kipya Manchester City katika kipindi hiki cha majira ya joto huku akiwa ametwaa mara tatu taji la Bundesliga katika misimu yake mitatu ya kuifundisha timu hiyo.
Kocha huyo wazamani wa Barcelona hakuwa katika furaha wakati mchezo hu ukianza kutokana na timu yake kutolewa na Atletico Madrid kwa sheria ya bao la ugenini katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Lakini kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 naye alikuwa na furaha kubwa wakati akishangilia na wachezaji wake baada ya filimbi ya mwisho dhidi ya Ingolstadt iliyopo katikati ya msimamo wa ligi baada ya kushinda mara 81 katika michezo 101 chini ya Guardiola.

Yanga yatanguliza mguu mmoja makundi Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuikandika Esperanca ya Angola 2-0



Na Mwandishi Wetu
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa Yanga (pichani), leo wamejiweka katika mazingira mazuri ya kucheza hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya kuisasambua GD Esperanca ya Angola katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kushinda mabao 2-0.

Mashujaa wa Yanga katika mchezo huo ni Simon Msuva na Matheo Antony Simon, baada ya kufunga mabao hayo katika kipindi cha pili cha mchezo huo, ambao unaiweka Yanga katika nafasi nzuri zaidi ya kutinga hatua ya makundi.

Kwa ushindi huo, vijanao hao wa Jangwani sasa wanahitaji sare, au ushindi wa aina yoyote na hata kufungwa 1-0 au kufungwa 2-1 ili kutinga wiki ijayo baada ya mchezo huo wa marudiano utakaofanyika Mei 17 Angola.

Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akimtoka beki wa Sagrada Esperanca, Antonio Kasule

Katika mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi kutoka Ghana, Joseph Lamptey aliyeuwa kati akisadiwa na David Laryea na Malik Salifu walioshika vibendera, Yanga walipoteza nafasi kibao za wazi za kufunga katika kipindi cha kwanza.

Kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Amissi  Tambwe ndiye aliyekosa mabao mengi baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi katika kipute hicho cha leo jijini Dar es Salaam.

Hatimaye chipukizi wa Yanga, Msuva na Matheo wakapeleka raha katika mitaa ya Jangwani Twiga baada ya kufunga mabao hayo mawili yaliyowanyamazisha kabisa Waangola.

Msuva alianza dakika ya 72 akimalizia krosi maridadi ya winga Godfrey Mwashiuya aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Malimi Busungu, kabla ya Metheo kufunga la pili dakika ya 90 kwa shuti la mbali. 

Pamoja na ushindi huo, Yanga ilionekana kabisa kuathiriwa na kuwakosa nyota wake wawili Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma ambao walikuwa wanatumikia adhabu za kadi za njano walizopewa mfululizo kwenye mechi dhidi ya Al Ahly mwezi uliopita.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela/Mbuyu Twite dk46, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Malimi Busungu/Godfrey Mwashiuya dk53, Amissi Tambwe na Deus Kaseke/Matheo Anthony dk77.

GGM, Tacaids wamteua Mrisho Mpoto `Mjomba' kuwa Balozi wa kampeni ya Kili Challenge


Mrisho Mpoto akisaini mkataba wa kuwa Balozi wa Kili Challenge.

Na Mwandishi Wetu
MGODI wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa Kushirikiana na Tume ya Kupambana na Ukimwi nchini (Tacaids) imemteua msanii maarufu wa mashairi Mrisho Mpoto kuwa balozi wa kampeni ya Kili Challenge.

Hafla hiyo ilifanyika katika ofisi za GGM jijini Dar es Salaam, ambapo Mpoto alisaini mkataba wa mwaka mmoja kuwa balozi wa Kili Challenge.

Kili Challenge ni kampeni inayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wa mapambano dhidi  ya VVU na Ukimwi. Kampeni hiyo ilianza miaka 15 iliyopita na hufanyika kila mwaka kwa wadau mbalimbali kupanda mlima Kilimanjaro, ambapo kwa mwaka jana walipanda watu 39 na kuchangisha takribani bilioni 1.2, sehemu ya fedha itagaiwa kwa asasi mbalimbali za kiserikali na za kijamii wakati wa sherehe za uzinduzi rasmi za sherehe ya mwaka huu zitakazofanyika Mei 20 katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu Hassan.

Mpoto ameteuliwa kuwakilisha na kuitangaza kampeni hii ili kusaidiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, kupambana na janga hili la Taifa. Pia kwa kuwa ni msanii na kupitia kazi zake za sanaa na ushawishi wake ndani ya jamii ataweza kuihamasisha jamii ipasavyo kuona umuhimu wa kumaliza tatizo hili hasa katika masuala ya unyanyapa.
 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Fatma Mrisho, “Inakadiriwa kuwa watu milioni 1.6 nchini wanaishi na VVU na Ukimwi. Ugonjwa wengi umewaathiri zaidi vijana na watoto yatima zaidi ya milioni 1.3. Tunahitaji kubadilisha hali hii. TACAIDS kwa kushirikiana na mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na wadau wengine kwa kupitia mpango huu wa Kilimanjaro Challenge tunapenda kutoa mchango na ushirikiano wetu kwa Taifa ili kutunisha mfuko utakaowezesha kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo,”

“Napenda kuupongeza mgoni wa Dhahabu wa Geita kwa kushirikiana na wadau wengine kwa kuamua kwa dhati kwa kipindi cha miaka 15 kuwekeza katika mradi huu kwa kuuwezesha kuwa mradi wa kitaifa na si wa GGM, hivyo pamoja na balozi wetu hivi sasa Mpoto tuungane nao ili kuongeza chachu kwa wadau wengine kujitokeza kuongeza nguvu katika mapambana dhidi ya janga hili,” alisema Dk. Mrisho.

Mrisho Mpoto 'Mjomba' akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids nchiniDk.  Fatma Mrisho.
Aliongeza … “Kwa kushirikiana na Mpoto tunamatumaini ya kujenga timu imara yenye hamasa ya kutuma ujumbe popote Tanzania na duniani ili kupambana na janga hili. Tunatoa wito kwa makampuni na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wajitokeze ili kushirikiane kutunisha mfuko wa Kilimanjaro Challenge na mwishowe kufikia ndoto au malengo ya nchi yetu ya kuhakikisha tunakuwa na kizazi kisicho na maambukizi ya VVU na Ukimwi,” Bw. Saimon Shayo, Makamu Rais wa miradi endelevu wa Anglogold Ashanti (GGM).

Shayo alisisitiza kwa kusema “GGM iko tayari kushirikiana na wadau wengine nia ya dhati, kuungana pamoja kupitia mfumo wa Kili Challenge katika kuhakikisha maambukizi haya hayaendelei kuleta athari kwa jamii yetu kwa sababu serikali yenyewe haitaweza kutokomeza tatizo hili,”
 
Naye Balozi mpya wa Kili Challenge, Mpoto alisema “Nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuweza kutoa mchango wangu katika kuisadia jamii kuepukana na janga hili. Changamoto kubwa inayotokana na janga hili la VVU na Ukimwi ni ongezeko la maambukizi ya VVU kwa vijana ambao, ndio nguvu kazi ya Taifa letui pasipo kila mmoja wetu kujitoa kwa dhati hatutalimaliza janga hili.”

Pamoja na hatua kubwa zilizopigwa na serikali ikishirikiana na wadau, kumekuwepo na ongezeko la maelfu ya watoto yatima wanaohitaji misaada baada ya wazazi wao kufariki, wajane wasiokuwa na kipato, pamoja na wazee wanaolazimika kuwalea wajukuu walioachwa na watoto wao, ambao walifariki kutokana na ugonjwa huo ulisisitiza Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS.

Kilimanjaro Challenge ni mradi unaolenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa wa ukimwi na virusi vya ukimwi (VVU). Pia inalenga kuchangisha fedha ili kujenga timu itakayoendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Ili kuweza kuwa sehemu yawatakaopanda Mlima Kilimanjaro, kwa kupitia Kili Challenge mwaka huu, uwe mtu binafsi au kupitia shirika kulipia wafanyakazi wake kupanda mlima mchango ni $5,000 tu, ambazo zitalipia gharama za upandaji na kuchangia mfuko wa Kili Challenge.

Kilimanjaro Challenge imebakia kuwa chombo muhimu kinachoshirikiana na taasisi za nje na ndani ya nchi katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kwa jamii ya Kitanzania na dunia kwa ujumla ili kuwapa matumaini ya kuhakikisha jamii inabaki bila kuathiriwa na ugonjwa huo katika miaka ijayo. 

Mpango huo pia unalenga kusaidia serikali kukabiliana na VVU na Ukimwi sambamba na kutoa nafasi kwa watalii wa ndani kuupanda mlima Kilimanjaro.

KUHUSU Kili Challenge:
  Kwa maelezo zaidi tembelea tovuti ya www.anglogoldashanti.com na www.geitakilichallenge.com.
Mrisho Mpoto 'Mjomba' akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids nchini, Dk. Fatma Mrisho.
 

Mrisho Mpoto (katikati) pamoja na Makamu wa Rais GGM, Simon Shayo na Mkurugenzi wa Mtendaji wa Tacaids, Fatma Mrisho wakiwa wameshika mkataba wa kumfanya Mpoto kuwa Balozi wa Kili Challenge.

Mrisho Mpoto akizungumza na wanahabari wakati wa kusaini mkataba wa kuwa Balozi wa Kili Challenge. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk. Fatma Mrisho.