Tuesday 8 January 2019

Bonanza la Shimiwi Kufanyika Dodoma Mwezi Ujao

Mchezo wa netiboli nao utakuwepo katika bonanza hilo la michezo la Shimiwi.

Na Mwandishi Wetu
BONANZA la Michezo la Shirikisho ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (Shimiwi) litafanyika jijini Dodoma Februari 2 na 3 kwenye Uwanja wa Jamhuri, imeelezwa.

Tamasha hilo litatanguliwa na mkutano wa viongozi wa michezo, ambao ni wenyeviti na makatibu wa klabu za michezo za Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Shimiwi Moshi Makuka, mbali na mazoezi ya viungo na mbio za pole (jogging), tamasha hilo litahusisha michezo ya mpira wa miguu, netiboli na ule wa kuvuta kamba.

Makuka alisema katika taarifa hiyo ni matumaini yake kuwa waajiri watatoa ruhusa kwa wahusika ili kuhakikisha bonanza hilo la michezo linafana kwa kushirikisha watu wengi bila kukosa.
Mkutano huo utafanyika Februari Mosi kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufuatiwa na bonanza hilo litakalofanyika kwa siku mbili kuanzia Februari 2 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kuanzia saa 12:30 asubuhi.

Alisema kuwa waajiri mbali na kutoa ruhusa, pia wanatakiwa kuwapatia wafanyakazi wao nauli na posho ya kujikimu ili waweze kushiriki vizuri katika mkutano na bonanza hilo la michezo katika siku zilizotajwa.

No comments:

Post a Comment