Thursday 10 January 2019

JNIA Yajipanga Madhubuti Kiusalama

Mkurugenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo. 

Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam umesema kuwa umejipanga mathubuti kiusalama.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha wakati akitoa ufafanuzi kuhusu madai ya abiria kuchukua muda mrefu katika jengo la pili la abiria wakati wakiwasili kiwanjani hapo kabla ya kutoka nje ya jengo hilo.
Mbali na madai hayo, pia Rwegasha alitolea ufafanuzi madai ya msanii maarufu nchini Ray Kigosi kuwa aliibiwa raba na perfume kiwanjani hapo kutoka katika begi lake wakati akisafiri kwenda Dubai akitokea JNIA tarehe 3 Jan, 2019.
Alisema kuwa mtangazaji wa Radio Clouds, Ephahimu Kibonde alilalamika katika kipindi cha Jahazi kuwa, alitumia saa mbili kabla ya kutoka nje ya Kiwanja hicho baada ya kuwasili akitokea Afrika Kusini.
Kibonde alishangaa abiria raia wa Tanzania kuchukua muda mrefu Kiwanjani hapo wakati  alitakiwa kutumia muda mfupi kwa kuwa hana mambo mengi ya kukaguliwa,  tofauti na wale wanaotoka nje ya nchi.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Idara ya Uhamiaji JNIA, Kanankira Mbise (kuhoto) akizungumza huku Mkurugenzi wa kiwanja hicho, Paul Rwegasha akimsikiliza.
Rwegasha alisema kuwa JNIA imefungwa kamera za usalama za CCTV katika maeneo yote ili kuhakikisha usalama wa abiria na mali zao wakati wakiwasili au kuondoka nchini kupitia kiwanjani hapo.
 Alisema kuwa mbali na mifumo mathubuti ya ulinzi na usalama, pia uongozi wa kiwanja hicho unasera ya kutotoa msamaha kwa Mtumishi yeyote atakayefanya udokozi na uwizi wa mali za abiria, ambapo akibainika anapelekwa kwenye vyombo vya sheria na kufukuzwa kazi moja kwa moja.
“Kamwe hatutamvumilia mfanyakazi yeyote mwenye tabia za kidokozi, ambaye atabainika kuiba mzigo wa abiria, kwani tutamtimua mara moja, na hilo kila mfanyakazi analijua ipo katika sera yetu,, “alisema Rwegasha.
Damas Temba (kushoto), ambaye ni Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiwanjani hapo akizungumza sula la usalama.
Aliomba watu wanapopata matatizo au changamoto kiwanjani hapo, kwanza wawasiliane na uongozi wa kiwanja ili kupata ufafanuzi na utatuzi wa matatizo yao kwa haraka, ambapo mwenendo wake utaangaliwa kwenye kamera za usalama ambazo zipo tangu abiria akiingia kiwanjani hadi anapopanda ndege, badala ya kukimbilia kuandika kwenye mitandao ya kijamii, kwani kufanya hivyo sio tu kunadhalilisha kiwanja, bali na nchi nzima kwa ujumla.
Akizungumzia Jengo la tatu la abiria linalojengwa maeneo ya Kipawa, Rwegasha alisema kuwa wanatarajia kuanza kulitumia mara baada ya kukamilika kwani kwa sasa kuna maeneo yanaendelea na ujenzi, licha ya nje kuonekana kama jengo hilo limekamilka. Jengo hili linatarajiwa kukabidhiwa kwa serikali Mei 2019.
Naye Kanankira Mbise, ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Idara ya Uhamiaji kiwanjani hapo alisema kuwa, idara yake imekuwa ikihakikisha inafanya shughuli zake kwa haraka na kufuata taratibu ili kuondoa msongamano wa abiria wanaowasili kutoka nje ya nchi.
Kwa upande mwingine, naye Damas Temba, ambaye ni Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiwanjani hapo alisema wananchi wanatakiwa kupata elimu zaidi ya kodi, kwani kuna vitu vikiingizwa nchini lazima vilipiwe kodi, hata kama ni zawadi, ambazo zikiwa ni nyingi.
“Abiria wanaosafiri na usafiri wa ndege wasione eneo la Forodha kama ni adui watoe ushirikiano kwa kuwa wakweli wa vitu walivyobeba, kwani hata zawadi zinalipiwa ushuru, mfano mtu anaweza akawa na begi lililojaa nguo na kudai ni zawadi, au saa za mkononi zaidi ya tatu, zipo sheria kabisa zenye kuonesha na kuzungumzia hili,” amesisitiza Temba.
Pia alisema mizigo lazima ikaguliwe kwa ajili ya usalama na mambo mengine, lakini wanajitahidi kufanya mambo kwa haraka ili kuepusha msongamano wa watu katika eneo la Forodha.
Hatahivyo, katika kipindi cha jana Jumatano cha Jahazi katika Radio ya Clouds, Kibonde alionekana kushangazwa tena na maelezo ya Temba kuwa hata zawadi  zinatozwa kodi.

No comments:

Post a Comment