Monday, 27 July 2015

Dk. Salim awataka Watanzania kulinda amani na utulivuNa Mwandishi Wetu
WATANZANIA wameaswa kulinda amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais mwezi Oktoba.

Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim kwenye ufunguzi wa Semina ya  siku tatu ya Urithi wa Utamaduni wetu iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha kiislam (Muslim University of Tanzania)  kupitia taasisi yake ya Urithi wa Utamaduni (Institute of Cultural Heritage).

“Cha msingi kuelekea uchaguzi mkuu, niwaombe watanzania kulinda amani na utulivu kwenye nchi yetu ili kuendeleza sifa hii nzuri inayotambulika kimataifa.

“Sasa tusiridhike na kujisahau tukaacha amani tuliyonayo ikapotea, ni muhimu kulinda amani ya nchi yetu, tusichukulie yanayotokea katika nchi nyingine ni ya uko uko tu, wote tuna wajibu wa kulinda amani ya nchi,”alisema Dk Salim ambae pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Dk  Salim alisema kwamba demokrasia imekuwa kwa kiwango kikubwa na hiyo inafanya watu kuwa na fikra tofauti na kusisitiza kwamba hakuna budi kukubaliana na fikra tofauti kwani ni matokeo ya kukuwa na kupanuka kwa demokrasia nchini.

“Kuna vyama vingi vya siasa nchini, vikubwa na vidogo, yote ni kutokana na kukua kwa demokrasia, uwingi wa vyama hivi unakuja na mawazo na fikra tofauti tofauti na hivyo hatuna budi kukubaliana navyo kwani wote ni watanzania,”alisema Dk Salim.

Alisema kwamba taifa linakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maadili unayofanya watu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa lengo la kwenda kula na sio kuwatumikia watanzania na kusema hali hiyo sio vyema ikiachwa iendelee kwa mustakabali mzuri wa taifa.

No comments:

Post a Comment