Sunday, 9 September 2018

Mkurugenzi Mkuu TAA, Bw. Mayongela Aongoza Waombolezaji Kuaga Mwili wa Mfanyakazi JNIA




Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Bw. Richard Mayongela akimpa pole mjane wa Marehemu Bw. Charles Salim nyumbani kwake Chang’ombe jijini  Dar es Salaam.
Na MwandishiWetu
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela leo meongoza mamia ya Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kuuaga mwili wa Ofisa Usalama Mwandamizi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), aliyefarikijuzi Tarehe 6/9/2018 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupatwa na shambulio la moyo.

Akisoma wasifu wa marehemu, Bw. Mayongela amesema Mamlaka itaendelea kushirikiana na familia ya marehemu, ambaye ameacha mjane na watoto wawili.
“TAA kama mwajiri wa marehemu tumefanikisha shughuli zote za hapa msibani natupo tayari kushirikiana na familia ya marehemi hata baada ya msiba huu kumalizika, "alisema Mayongela.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Bw. Richard Mayongela akitoa salamu za rambimbi katika msiba wa Bw Charles Salim Chang'ombe Jijini Dar es Salaam.
Bw.Mayongela amesema marehemu wakati wa uhai wake alifanyakazi kwa ufanisi mkubwa, hivyo ameacha pengo kubwa kwa taasisi.

Naye msemaji wa Familia, Bw. Herbert Semwaiko aliishukuru TAA kwa ushirikiano walionesha tangu kuugua ghafla kwa marehemu hadi kufariki kwake.

“Sina maneno zaidi ya kusema pamoja na Kiswahili ni lugha pana zaidi, ila nasema asante sana tunawashukuru kwa ushirikianowenu mliouonesha, ambapo mmetusaidia kuanzia mwanzo wa ugonjwa wa ghafla hadi kufariki kwake kijana wetu, Charles, "anasema Bw. Semwaiko.

Kwa upande wake, Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Daniel Mhando katika ibada yake fupi ya kumuombea marehemu aliwataka waombolezaji kumuombea katikasafari ya mwisho atazikkwa Jumapili Septemba 9, 2018 wilayani Muheza mkoani Tanga.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wakiwa na Mkurugenzi Mkuu (watatu kulia), Bwa. Richard Mayongela wakiwa pembeni ya jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Ofisa Usalama Mwandamizi, Bw Charles Salim tayari kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho.
Marehemu alizaliwa tarehe Oktoba 3, 1963 na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Kibasila Jijini Dar es Salaam na baadae elimu ya sekondari katika shule ya Hengongo mkoani Tanga, ambapo alihitimu kidato cha nne mwaka 1983 na mwaka 1984 aliajiriwa serikalini na kupangiwa kazi Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Dar es Salaam, kama Ofisa Usalama, na mwaka 2015 alipandishwa cheo na kuwa Ofisa Usalama Mwandamizi.
Watoto wa aliyekuwa Ofisa Usalama Mwandamizi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Charles Salim, James Charles (Mwenye fulana nyeusi) na Lissa Charles (aliyefunga kitambaa kichwani) mara baada ya ibada fupi wakiwa na Mkurugenzi Mkuuwa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wa pili kulia) nyumbani kwao Chang’ombe jijini  Dar es Salaam.
 Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa Jina Lake Lihimidiwe. Amina.

Thursday, 6 September 2018

Uchukuzi Sports Club Yaanza Maandalizi ya Shimiwi


1.        Wachezaji wa timu ya wanawake na wanaume ya kuvuta Kamba ya Klabu ya Uchukuzi (USC) wakifanya mazoezi jana nyuma ya jengo la Aviation Banana ya kujiandaa na mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), iliyopangwa kuanza Septemba 25 mkoani Dodoma.

Na Mwandishi Wetu
KLABU ya michezo ya Uchukuzi (USC), imeanza kujifua kwa ajili ya kushiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), itakayoanza Septemba 25 kwenye viwanja mbalimbali mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mbura Tenga amesema wameanza kujifua kwa nguvu ili kurudi na ubingwa wa michezo mbalimbali waliyoshinda kwa mara ya mwisho michezo hiyo ilipofanyika mwaka 2014.
Katibu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Vallery Chamulungu (wa kwanza kulia) akiwa ni miongoni mwa wachezaji wa klabu ya Uchukuzi walioanza mazoezi jana nyuma ya jengo la Aviation wakijiandaa na mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), iliyopangwa kufanyika mkoani Dodoma kuanzia Septemba 25, 2018.
Tenga amesema USC watashiriki kwenye michezo tisa, ambayo imeandaliwa na Shimiwi, ambayo ni mpira wa miguu, netiboli, kuvuta Kamba, riadha, bao, karata, draft, baiskeli na Darts.
   Sharifa Amiri (kulia) akifanya mazoezi ya mchezo wa bao na Bw. Ambakise Mwasunga jana kwenye  viwanja vya nyuma ya Jengo la Aviation wakijianda na mashindano ya Shirikisho la michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), iliyopangwa kuanza Septemba 25, 2018 mkoani Dodoma.
“Tunauhakika wa kwenda kufanya vizuri kwani timu imeanza mazoezi tayari ingawa muda ni mdogo, ila ninaamini tutafanya vizuri,” amesema Tenga.

USC inatetea vikombe vinne walivyoshinda mwaka 2014, ambavyo ni Darts – wanaume (washindi wa kwanza); mpira wa miguu (washindi wa pili); na Kamba – wanaume na baiskeli - wanawake (washindi wa tatu).
Katibu Mkuu wa Klabu ya Uchukuzi (USC), Mbura Tenga (katikati) jana akijumuika na wachezaji wa klabu hiyo kwenye viwanja vilivyopo jirani na jengo la Aviation kufanya mazoezi ya kujianda na Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), iliyopangwa kufanyika mkoani Dodoma kuanzia Septemba 25, 2018.
Ratiba iliyotolewa na Shimiwi inaonesha katika ufunguzi mabingwa watetezi katika mchezo wa kuvuta Kamba wanaume timu ya Ofisi ya Rais Ikulu itavutana na MSD; nao wanawake wa RAS Iringa ambao ni mabingwa watetezi watavutana na Viwanda; huku katika mpira wa miguu Wizara ya Elimu watakutana na Ukaguzi.
     Wachezaji wa mpira wa miguu wa Klabu ya Uchukuzi (USC) wakijifua kwenye viwanja jirani na Jengo la Mamlaka ya Mawasiliano ya Anga wakijiandaa na Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), inayotarajiwa kufanyika mkoani Dodoma kuanzia Septemba 25 hadi Oktoba 6, 2018.  
Michezo hiyo ambayo pamoja na kuunganisha wafanyakazi wa umma wa maeneo mbalimbali pia huleta burudani kwa wakazi wa eneo husika.


Saturday, 1 September 2018

TAA Yachangia Vyoo Salama kwa Mtoto wa Kike


1.   Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kulia) akiwaongoza Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo, Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha (katikati) na Ofisa Uhusiano, Bi. Bahati Mollel (wapili kulia) kukabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh Mil 5 Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Makinda (wapili kushoto) na Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya hafla hiyo, Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka. Hafla hiyo ilifanyika jana usiku kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.



Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeunga mkono juhudi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Umoja wa Wabunge Wanawake wa Bunge hilo (TWPG) kukusanya fedha kwa ajili ya kujenga vyoo salama vya shule nchi nzima kwa ajili ya mtoto wa Kike kwa kutoa mchango wa kiasi cha Sh Mili 5.

Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela, alikabidhi msaada huo wa fedha kwa mgeni rasmi, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Makinda.

Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyoudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Wabunge, Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, aliwapongeza Wabunge hao kwa hatua hiyo ya kuhakikisha kunakuwepo kwa mazingira bora shuleni ili kutoa haki sawa ya kupata elimu kwa wanafunzi wa jinsia zote.

“Wazo hili litasaidia sana serikali katika kuhakikisha mazingira ya shule yanaboreshwa ili kutoa nafasi sawa kwa wanafunzi wote wa kike na kiume,” alibainisha Spika Ndugai.

Alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli, amefurahishwa na kitendo hicho na kwamba ameshindwa kuhudhuria hafla hiyo kwa vile bado yupo kwenye msiba wa dada yake huko Chato mkoani Geita.

Kwa upande wake, mgeni rasmi Mhe. Anne Makinda aliwapongeza Wabunge hao wanawake kwa hatua hiyo ya kuunga mkono juhudi za serikali na kuwataka Wabunge wanaume kuwaunga mkono wenzao katika kufanikisha kampeni hiyo inayolenga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.5 zitakazowezesha kujenga vyoo salama vya shule kwenye majimbo yote 264 nchi nzima.
Taasisi Mbalimbali zilichangia kwenye harambee hiyo, ambapo pia vitu mbalimbali vilinadiwa na fedha zitakazopatikana zitakwenda kufanya kazi ya ujenzi huo.