Saturday, 11 July 2015

Iker Casillas aondoka Real Madrid baada ya kuichezea kwa miaka 25



Kipa Iker Casillas.
MADRID, Hispania
KLABU ya Porto imekubali mpango wa kumsajili kipa wa Hispania Iker Casillas kutoka Real Madrid.

Casillas,mwenye umri wa miaka 34, aliyebakisha mwaka mmoja aktika mkataba wake, anaondoka Real baada ya miaka 25, ambapo katika kipindi chake alitwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na matano ya La Liga.

Mchezaji huyo anashikilia rekodi ya Hispania kwa kucheza mechi 162 katika timuyake ya taifa na kushinda taji la Ulaya pamoja na lile la dunia.

Kipa wa Manchester United David De Gea, 24, amekuwa akihusishwa na kuhamia Madrid kumbadili Casillas.

Casillas alijiunga na shule ya soka ya Real mwaka 1990, na kuichezea kwa mara ya kwanza mwaka 1999 na kutumia muda wake eote katika klabu hiyo, na kutwaa mataji 17 makubwa.

Aliondolewa katika kikosi cha kwanza na Jose Mourinho katika msimu wa mwaka 2012-13, huku kocha huyo Mreno akimpa nafasi zaidi Diego Lopez.

Katika msimu wa mwaka 2013-14 kocha Carlo Ancelotti alimchezesha Casillas peke yake katika mechi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na zile za Kombe la Mfalme wakati Real Madrid ikitwaa taji lake la 10 la Ulaya.

Msimu uliopita alichukuliwa kama kipa namba moja lakini ujio wa De Gea unatarajia kumbadili kama kipa namba moja katika Reak madrid na Hispania.

Mataji ya Casillas

3 x Ligi ya Mabingwa (2000, 2002, 2014)
    
2 x Kombe la Mfalme (2011, 2014)
5 x La Liga (2001, 2003, 2007, 2008, 2012)
1 x Klabu Bingwa ya Dunia (2014)
1 x Kombela Dunia (2010)
2 x Kombe la Ulaya (2008, 2012)

Kwaheri ya kuonana:-

Taarifa kamili ya Real Madrid kuhusu kuondoka kwa Casillas:

"Kwa Real Madrid leo ni sikukubwa kuliko zote, kwa ajili ya kushukuru na kutambua mchango wake. Mmoja kati ya makipa bora katika klabu hii sio tu anaondoka, leo kipa bora zaidi katika historia ya klabu na katika historia ya soka la Hispani anaondoka katika hatua mpya ya historia ya maisha yake ya soka.

"Iker Casillas alifanya mambo mengi pamoja na kuwa nahodha wetu na amekuwa gwiji tangu alipowasili hapa kama mtoto akiwa na umri wa miaka tisa ru.

Klabu yetu ina umri wa miaka 113 na Casillas amekuwa akivalia jezi namba 25 katika miaka hiyo. Wakati wa kipindi hicho amekuwa mmoja wa viongozi wazuri na alipata heshima kubwa na upendo kutoka kwa mashabiki.



"Iker anaondoka, lakini urithi wake utakuwa hapa milele. Mipango yake na uchezaji wake katika mechi 725 aliyecheza ndani ya jezi yetu inangara kwa wale wote wenye ndoto ya kuwa sehemu ya timu hii.

"Ahsante kwa yote Iker uliyofanya. Ahsante kwa kuwa alama ya ubora katika historia yetu. Unaondoka lakini kwa kweli kamwe hatutakusahau na siku zote utakuwa katika moyo wa Real Madrid."

Gerrard aanza kwa kishindo katika timu yake mpya ya La Galaxy


Nahodha wazamani wa Liverpool, Steven Gerrard akicheza katika timu yake mpya ya La Galaxy.

NEW YORK, Marekani
STEVEN Gerrard alicheza dakika 45 akiichezea kwa mara ya kwanza timu yake ya Marekani ya LA Galaxy wakati ikitoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Club America katika mashindano ya Kombe la Kimataifa.

Mchezaji huyo wazamani wa Liverpool kwa mara ya kwanza alivaa jezi ya klabu tofauti baada ya miaka 27 huku akionesha mchezo wa kuvutia wakati mabao ya mchezo huo yakifungwa na Robbie Keane na Alan Gordon.

Gerrard pamoja na kucheza dakika 45 tu lakini alionesha mchezo wa kuvutia kama ilivyotarajiwa na wengi na karibu alipatie bao timu yake lakini shuti lake la karibu liliokolewa na Hugo Gonzalez.

Friday, 10 July 2015

Yanga imekamilika kwa michuano ya Kombe la Kagame




Kikosi cha Yanga Africans.
Na Mwandishi Wetu
KOCHA mkuu wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, Hans van der Pluijm amesema kuwa, licha ya kupata ushindi mdogo wa 1-0 dhidi ya KMKM ya Zanzibar juzi kwenye Uwanja wa Taifa, lakini kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame.

Pluijm alisema licha ya upungufu mdogo uliojitokeza, ana matarajio makubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na hata kulibakiza kwenye ardhi ya Tanzania kombe hilo ambalo linawaniwa na timu 13.

Michuano ya Kombe la Kagame inatarajia kuanza jijini Dar es Salaam Julai 18 kwenye Uwanja wa Taifa.

Akizungumza juzi Pluijm alisema kikubwa kilichomvutia katika mechi tatu za kirafiki walizocheza ni namna ambavyo timu hiyo ilivyokuwa na uwiano baada ya kuziba nafasi za wachezaji ambao wameachana nao baada ya msimu uliopita kumalizika.

Naweza kusema hiki ndicho kikosi changu bora ukilinganisha na kile kilichobeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kila mchezaji tuliyekuwa naye msimu huu ana kitu cha ziada na wamekuwa na ushirikiano mzuri pamoja na wale wageni, alisema Pluijm.

Mholanzi huyo pia alisema amefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na mshambuliaji mpya raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma ambaye ndiye aliyefunga bao hilo pekee katika mchezo na KMKM na kusema atakuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi chao na ni mmoja ya washambuliaji anayemtegemea kufunga mabao mengi msimu huu.

Waturuki watoa futari ya zaidi ya Sh. Milioni 30 kwa wa kazi wa Dar



Wafanyakazi wakishusha maboksi yenye futari kwa ajili ya Waislamu wa Ilala jijini Dar es Salaam. Kulia ni  Mwenyekiti wa taasisi ya Forum For Balance and Sustainable Development, Imamu Faraji Tamimu akisimamia zoezi hilo.


Mratibu wa dini wa ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania, Muhammed Cicek (wa pili kushoto) wakati ugawaji wa futari kwa wakati za Ilala jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanawake wa Kiislamu wa Ilala wakisubiri kukabidhiwa futari zao zilizotolewa na ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa taasisi ya Forum For Balance and Sustainable Development, Imamu Faraji Tamimu (kushoto) akizungumza jambo wakati wa utoaji wa futari hizo.
 
 
 
 
Na Seba Nyanga
WAISLAMU wa Uturuki kupitia ubalozi wao nchini Tanzania wametoa futari yenye thamani ya zaidi ya sh. Milioni 30 katika mkoa wa Dar es Salaam, imeelezwa.

Kwa mujibu wa mratibu wa dini wa ubalozi wa Uturuki nchini, Muhammed Cicek, futari hiyoitawanufaisha waumini wa Kiislamu 1800 wa wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke.

Alisema kila wilaya waumini 600 wamefaidika na zoezi hilo ambalo kwa upande wa Ilala lilifanyika katika msikiti wa Masjid Taqwa, ambapo mwakilishihuyo aligawa maboksi ya futari kwa waumini hao.

Akizungumza kabla ya kugawa futari hiyo mwakilishi huyo aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu kuwa na mshikamano miongoni mwao na kuwasaidia wasiojiweza kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akigawa chakula hicho kwa niaba ya taasisi ya Hasene ya Uturuki,   Cicek alisema kwamba wametoa msaada huo sio kwa sababu ya uwezo mkubwa wa kifedha waliokuwa nao ama umasikini wa Watanzania, bali kuendeleza mshikamano miongoni mwa waumini wa Kiislamu Tanzania.

Cicek aliwataka waislamu wa Tanzania kuwaombea waislamu wengine wanaopoteza maisha kwenye nchi za Palestina, Syria, Iraq na kwingineko.

Naye Mwenyekiti wa taasisi ya Forum For Balance and Sustainable Development, Imamu Faraji Tamimu alitoa rai kwa waislamu nchini kote kuendelea kuwaombea wenzao wa Uturuki kupitia taasisi yao ya Haseni kwa msaada wa chakula walioutoa wakati huu wa Ramadhani.

Wenzetu wa Uturuki wametupa msaada huu sio kwa sababu ni matajiri ila kwa sababu ya moyo wa upendo kwa Waislamu wenzao, alisema Imamu Tamimu.