![]() |
Wajumbe wa Kamati ya Michezo ya mashindano
ya Mei Mosi wakiwa kwenye kikao cha Kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo
kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro
TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) mkoa wa Mwanza
itashirikishwa kwenye Michezo ya Mei Mosi inayotarajiwa kuanza Aprili
16-29, 2020 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo, endapo kutakuwa na timu
za Wizara, Taasisi za Umma na Binafsi zitawatumia
wachezaji wasiokuwa watumishi wao halali.
Katibu
wa Kamati ya michezo hiyo, Moshi Makuka, alisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye
kikao cha kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro, ambapo suala hilo
limewekwa kwenye kanuni namba 13 kati ya 15 zilizopitishwa na wajumbe wote
walioshiriki kwenye kikao hicho.
Makuka
alisema mbali na Takukuru kushirikishwa kubaini uhalali wa mchezaji
aliyesajiliwa na timu iliyomchezesha, pia viongozi wote walioshiriki kumsajili
mchezaji huyo wataripotiwa kwenye taasisi hiyo, ili sheria za nchi zichukue
mkondo wake.
![]() |
Katibu Mkuu wa Kamati ya Michezo ya mashindano
ya Mei Mosi, Moshi Makuka (aliyenyoosha
mikono) akisisitiza jambo kwenye kikao cha Kwanza cha maandalizi ya michezo
hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) Mkoani Morogoro
“Haya
mashindano yanajumuisha watumishi halali wa taasisi na wizara hivyo hairuhusiwi
kuwachezesha wachezaji ambao sio watumishi halali, kwa lengo la kujipatia
ushindi, hili ni katazo na kanuni yetu ipo wazi kabisa, hivyo timu zisithubutu
kuja na wachezaji hao kabisa,” alisisitiza Makuka.
Alizitaja
adhabu ambazo timu itakayobainika kumtumia mamluki ni pamoja na viongozi wake
watafungiwa kushiriki michezo hiyo kwa muda wa miaka miwili na nakala ya barua
itawasilishwa kwa Mwajiri wake; timu itatozwa faini ya Tshs. 500,000; timu husika itapokonywa
ushindi endapo itakuwa imeshinda; timu itaondolewa kwenye mashindano.
Kamati
imesema mamluki wanadhibitiwa kwa wanamichezo kuwa na vitambulisho halisi vya
kazi, Kadi ya Bima ya Afya, Kadi ya Mfuko wa Jamii na hati ya Malipo ya
mshahara za miezi miwili ‘salary slip’.
Hatahivyo,
Makuka alisema timu zote shiriki zinatakiwa kuwahi mkoani Mwanza tarehe 14
Aprili, 2020 ambapo ndipo sherehe za Sikukuu za wafanyakazi zitafanyika Kitaifa
kama ilivyotangazwa awali, ambapo timu itakayochelewa hadi tarehe 20 Aprili,
2020 itakuwa imejiondoa kwenye michezo hiyo.
“Timu
ikichelewa inawapa shida na kuwaumiza wachezaji kwa kuwa watacheza mfululizo
ili kwenda na ratiba, hadi kufikia michezo yao iliyosalia, hivyo hii hatutaki
kwani michezo itakuwa haina ushindani kwa kuwa wachezaji wa timu moja watakuwa
wamechoka kwa kucheza mfululizo wa mechi mbili au tatu kwa siku, hivi huu ni
mwezi wa pili muanze kufuatilia ruhusa za wachezaji wenu,” alisema Makuka.
Kamati
inategemea ushiriki wa timu zaidi ya 25, kwa kuwa zinaongezeka kila mwaka
ambapo mwaka jana zilishiriki timu 23. Michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na
soka, netiboli, kuvuta kamba, baiskeli, riadha, karata, bao na draft.
Pia
Makuka amesisitiza timu shiriki kulipa ada ya ushiriki kwa wakati, ili fedha hizo
zitumike katika ulipaji wa gharama mbalimbali za uendeshaji wa mashindano hayo.
Ada
ya ushiriki ni Tshs. 1,000,000 ambapo kila timu inatakiwa kulipa mapema kabla
ya tarehe 6 Aprili, 2020, ili timu ziweze kupewa kadi za ushiriki
zitakazofanikisha usajili wao.
Halikadhalika
Makuka amesema timu zote zilizotwaa vikombe kwa kuwa washindi wa Kwanza hadi wa
tatu wanatakiwa kurejesha vikombe walivyoshinda kabla yatarehe 29 Machi, 2020
na timu itakayochelewa utatozwa faini ya Tshs. 200,000.
Wakati
huo huo, Makuka amesema timu zinaruhusiwa kushiriki kwenye michezo ya
mashirikisho mbalimbali yakiwemo ya Shimiwi, Shimmuta na Mei Mosi, na sio
kusubiri michezo ya shirikisho moja, ambayo kwa wakati huo inakuwa haijafanyika
kwa sababu mbalimbali.