Thursday, 2 February 2017

TOURE AONGEZWA KATIKA KIKOSI CHA LIGI YA MABINGWA WA ULAYA



MANCHESTER, England
KIUNGO Yaya Toure (pichani), ameitwa katika kikosi cha Manchester City kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Toure, 33, aliachwa katika kikosi cha wachezaji 25 katika hatua ya makundi, lakini tangu wakati huo amekuwa akicheza katika kikosi cha kwanza, na amechukua nafasi ya majeruhi Ilkay Gundogan.

Mchezaji mpya Gabriel Jesus, aliyefunga wakati Man City ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya West Ham juzi Jumatano, aliingia akichukua nafasi ya Kelechi Iheanacho.

City itakabiliana na Monaco katika hatua ya 16 bora, ambapo mchezo wa kwanza utachezwa Februari 21.

Kuondolewa kwa Toure katika hatua hiyo ya makundi kulikosolewa na wakala wake Dimitri Seluk, na kocha wa Man City Pep Guardiola alisema hatampanga kiungo huyo hadi atakapoomba radhi.

Novemba, mchezaji huyo bora mara nne wa mwaka wa Afrika aliomba radhi na kurejeshwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

TIMU TANO ZAFUZU SITA BORA LIGI KUU YA WANAWAKE TANZANIA BARA



Na Mwandishi Wetu
TIMU tano zimefuzu hatua ya sita bora ya Ligi ya Wanawake Tanzania Bara baada ya hatua ya makundi, wakati mechi za mwisho zitaamua timu ya mwisho ya kukamilisha hatua hiyo.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas ameiambia leo Bin Zubeiry Sports – Online kwamba kutoka Kundi B timu zote tatu za kusonga sita bora zimekamiliaa mbazo ni JKT Queens ya Dar es Salaam, Mlandizi Queens ya Pwani na Fair Play ya Tanga. 

Timu zilizikosa nafasi ya kusonga mbele kutoka kundi hilo ni Evegreen ya Temeke, Mburahati Queens ya Dar es Salaam na Viva ya Mtwara.Lucas alisema timu zilizofuzu hadi sasa kutoka Kundi A ni Sisters ya Kigoma na Marsh Academy ya Mwanza.

 Timu nyingine zilizobaki ambazo zinawania nafasi moja ya kukamilisha timu za kufuzu Sita Bora kutoka kundi hilo ni Panama ya Iringa, Baobab ya Dodoma, Majengo ya Singida na Victoria na Queens ya Kagera.

Hatua ya Sita Bora inatarajiwa kuanza katikati ya mwezi Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na bingwa atajainyakulia Kombe na Medali za rangi ya Dhahabu, mshindi wa pili Kombe na Medali za rangi ya Fedha.

Wednesday, 1 February 2017

MBOMA AIONYA GHANA KUTOIDHARAU CAMEROON NUSU FAINALI AFCON KESHO


Mashabiki wa Cameroon wakishangilia katika moja ya mechi za timu yao.

LIBRAVILLE, Gabon
MCHEZAJI bora wazamani wa mwaka wa Afrika, Patrick Mboma, ameionya Ghana kutoidharau Cameroon katika mchezo wao wa nusu fainali utakaofanyika kesho Alhamisi.

Mboma  ni mchezaji wazamani wa kimataifa wa Cameroon aliyeichezea nchi hiyo kwa mafanikio makubwa.
Mchezaji huyo bora wa Afrika wa mwaka 2000 anasema kuwa Ghana inapewa nafasi kubwa ya kucheza fainali ya mashindano hayo kutoka na uzoefu na kiwango cha wachezaji wake.

Lakini mchezaji huyo aliigeukia timu hiyo na kuitaka kutoidharau hata kidogo Cameroon ambayo inaweza kuwa tatizo kubwa kwa Black Stars.

Mboma alisema, “Nina furaha kuona timu ya Cameroon yenye kujiamini na zaidi, yenye mawazo mazuri katika nusu fainali ya mashindano haya, na hata kama timu hiyo ilikuwa haitarajiwi kufika hapo.”

Timu hiyo ya Cameroon sio miongoni mwa timu zilizokuwa zikipewa nafasi ya kufanya vizuri kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

Cameroon iliifunga Senegal iliyokuwa ikipewa nafasi ya kufanya vizuri na sasa Cameroon wamo katika mbio za ubingwa.

Mpambano huo wa leo utakaofanyika Franceville utakuwa ni mrudiano wa nusu fainali ya Afcon wa mwaka 2008 Afcon, ambako Cameroon iliifunga Ghana kwa bao 1-0 jijini Accra na kucheza fainali yao ya mwisho ya mashindano hayo.

Zote Ghana na Cameroon kila moja imetwaa mara nne taji la Afcon, ambapo kila moja anataka kuongeza idadi hiyo ya mataji.

EMMANUEL OKWI ASAINI CLUB SPORTS VILLA, KIIZA AMWAGA WINO URA



KAMPALA, Uganda
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda Emmanuel Okwi aliyekuwa anakipiga kwenye klabu ya Ligi Kuu ya Denamark ya SønderjyskE, amejiunga na klabu ya Sports Club Villa ya nchini kwao Uganda.

Mshambuliaji huyo aliyeanza maisha yake ya soka kwenye klabu ya Sports Club Villa anarejea kwenye klabu hiyo kwa mkataba wa muda mfupi ambao utamfanya achezee klabu hiyo mpaka mwishoni mwa msimu huu.

Okwi  aliondoka  SC Villa na kujiunga na Simba mwaka 2010 baada ya kuisaidia timu hiyo ya Uganda kushinda taji la nchi hiyo mwaka 2009.

 “Usajili wake umekamilika,” alithibitisha Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo,  Ivan Kakembo .

Usajili wa mshambuliaji huyo kunaweza kuwa pigo kwa klabu ya Simba ambapo iliriafiwa kuwa na mpango wa kumrejesha kuimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwa msimu ujao.

Hata hivyo Simba bado inaweza kumpata mshambulaji huyo mwishoni mwa msimu huu kama hataamua kusaini kusaini mkataba mpya na klabu hiyo pindi mkataba wake wa sasa utakapomalizika na Simba kama bado itaendelea kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo.

Wakati Okwi akirejea kwenye klabu yake ya zamani ya Sports Club Villa, swahiba wake mkubwa Hamisi Kiiza’Diego’ aliyewahi kutamba na mabingwa wa soka wa Tanzania Bara Yanga kabla ya kutimkia Simba nae amerejea kwenye klabu yake ya URA huko huko Uganda.

Kiiza amejiunga na URA akitokea klabu ya Free State ya Afrika Kusini aliyojiunga nayo Agosti mwaka jana baada ya kumaliza mkataba wake na klabu ya Simba, pia amesaini mkataba wa muda mfupi utakaomuweka kwenye klabu hiyo mpaka mwishoni  mwa msimu huu.

 “Najisikia vizuri kurudi nyumbani,” alisema Kiiza. “Nina kumbukumbu nyingi nzuri kwenye klabu hii na niko hapa kulipa shukrani kwa imani yao kwanguI,”aliongeza.

Kiiza alisema kuwa alikuwa na ofa nyingi kutoka ndani na nje ya Uganda lakini aliamua kurejea kwenye klabu aliyodai iko ndani ya moyo wake.
.