Friday, 1 December 2017

CAF yazipiga nyundo SuperSport na TP Mazembe

CAIRO, Misri
BODI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) limeziadhibu klabu za TP Mazeme na Supersport United baada ya mashabiki wao kuvamia uwanjani katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Jumamosi iliyopita.

Mchezo huo wa fainali uliofanyika Novemba 25 mwaka huu, ulipigwa kwenye Uwanja wa Lucas Moripe jijini Pretoria.

Kwa mujibu wa Ibara ya 83 na 151 ya Sheria za Caf, Supersport imepigwa faini ya dola za Marekani 15,000 kutokana na vurugu hizo za mashabiki.

Klabu hiyo ya Afrika Kusini pia imeonywa kutorudia kosa kama hilo, au watajikuta wakipewa adhabu ya kucheza bila mashabiki.

Kwa upande wa TP Mazembe, wenyewe wamepigwa faini ya dola za Marekani 5,000 kutokana na tabia za mashabiki wao, ambao walikiuka sheria namba 82 na 83 ya sheria za Caf.

Katika mchezo huo, TP Mazembe ya Congo ilifanikiwa kutetea taji lake iliyoshinda mwaka jana baada ya kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 2-1 baada ya kuilazimisha sare ya bila kufungana Supersport katika mchezo huo wa marudiano.


Katika mchezo wa kwanza, TP Mazembe ilitumia vizuri uwanja wake wa nyumbani na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment