Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela
amewataka madereva wanaoendesha magari ya zimamoto na uokoaji kwenye
viwanja vyote vya ndege Tanzania kuyathamini na kuyatunza magari hayo kwa kuwa
wameaminiwa kufanya kazi hiyo.
Bw. Mayongela alitoa kauli hiyo kwenye Kituo
cha Zimamoto na Uokoaji cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), alipokwenda kujitambulisha na kujadili changamoto mbalimbali
zinazowakabili, ambapo alisema magari hayo yamenunuliwa kwa gharama kubwa,
hivyo yanapaswa kutunzwa.
Alisema uthamini wao kwa magari hayo
kutayafanya kudumu na kuyafanya kazi kwa muda mrefu bila kuharibika, jambo
ambalo litachangia ufanisi wa kazi, ya uokoaji na usalama kwenye viwanja vya
ndege, ambapo mbali na miundombinu pia lazima miundombinu ipewe kipaumbele.
“Najua wapo wenzenu wachache sio waaminifu
wamekuwa wakitengeneza manunuzi hewa ya vifaa na hata mafuta kwa manufaa yao
binafsi, lakini ninawaomba mujione nyie ndio wenye thamani kwa kuaminiwa kuendesha
magari haya ya mamilioni ya fedha, kwani ni nyie tu mnayoweza kuyaendesha
kutokana na kuwa na mitambo ya kisasa tofauti kidogo na mengine, hivyo basi
tuyatunze ili tuisaidie serikali yetu isiingie gharama za mara kwa mara za
kununua vifaa au magari mengine mapya,” alisisitiza Bw. Mayongela.
Hatahivyo, alisema zimamoto ni moja ya mambo
ya msingi hivyo amewahakikishia kuwapeleka kozi za mara kwa mara za ndani na
nje ya nchi, kutokana na mambo mbalimbali yanayobadilika duniani, na kwa
kuanzia ataanza na askari wawili hadi wanne, kulingana na mafunzo wanayostahili
kushiriki, na atahakikisha washiriki ndio wanaokwenda kufanyia kazi kwa vitendo
katika utendaji wao na sio kupeleka mabosi ambao hawahusiki.
“Nia yangu ni nyie kufanya kazi kwa weledi na
kufanyakazi kwa bidii, nisije kusikia hakuna fedha, lakini wakati huo huo
mnamuona Mkurugenzi Mkuu anapanda ndege kwenda Ulaya na kurudi hizo fedha
zinatoka wapi, nasema kama kweli kuna mambo ya msingi basi Zimamoto ni jambo la
msingi, hivyo basi sisi wafanya maamuzi tunatakiwa kuangalia wanaostahili
kupata mafunzo na waende, hivyo nitahakikikisha kwa kadri ya bajeti nitatenga
mafungu ya kupeleka watu wangu hawa kwenye mafunzo, ili nao waende na wakati
katika endeshaji kulingana na mabadiliko ya teknolojia na mashirika ya usafiri
wa anga duniani yanavyoagiza,” alisema Bw. Mayongela.
Hatahivyo, ameahidi kwa mwaka wa fedha
2017/2018 TAA itanunua magari sita ya zimamoto na uokoaji pamoja na redio
zitakazotumika kwa mawasiliano katika chumba cha habari na mawasiliano,
kinachowasiliana na mnara wa kuongoza ndege.
Kutokana
na kuharibika kwa mara kwa mara kwa magari ya Zimamoto kwenye viwanja
vya ndege, Tanzania ameahidi kufufua karakana ya kutengeneza magari hayo iliyopo
JNIA, ambapo tayari amewaita mafundi waliopo hapo kukutana naye ili kuwasilisha
changamoto na vifaa vinavyohusiana na magari hayo, ili waanze kutengeneza kwa
haraka baada ya kununuliwa vifaa hivyo.
Pia aliwataka kuwa na ushirikiano wa dhati na
wafanyakazi wa TAA katika utendaji wao wa kazi na kuwa walinzi wa mali za
serikali kutokana na wao wamekula kiapo.
Naye Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji wa
Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna Msaidizi Christom Manyologa alisema
amefarijika kwa ujio wa Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw. Mayongela, ambaye ameonesha nia thabiti ya kushirikiana
katika kazi.
Kamishna Manyologa alisema askari wa Zimamoto
na Uokoaji , astahili kuheshimika zaidi kwani yeye ndio anayeweza kuingia ndani
na kufika karibu ya ndege na pia anayewasiliana na waongoza ndege.
“Huyu askari anastahili kuheshimiwa kwanza
anamamlaka makubwa ya kuwa karibu kabisa ya ndege, kupita ndani ya barabara ya
kutua na kuruka kwa ndege, hivyo anaweza kufanya lolote baya akiamua, hivyo
watendewe vizuri,” alisema Kamishna Manyologa.
No comments:
Post a Comment