Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Mhe. Prof. Makame Mbarawa amewataka wadau wanaofanya shughuli mbalimbali
zinazohusisha na kodi ya pango kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Julius
Nyerere (JNIA), kuhakikisha ifikapo Februari 1, 2018 wawe wameshalipa madeni
yao.
Prof. Mbarawa alisema leo wakati alipoongea
na wadau hao kwenye ukumbi wa watu Mashuhuri wa JNIA-TBII, wakati
walipozungumza nao kujadili masuala mbalimbali.
Alisema baadhi ya wadau wameshalipa madeni
yao kati ya bil 10 zilizokuwa zinadaiwa na sasa zimesalia bil. 3.7 ambapo
amewataka baada ya kumalizika kwa sherehe za Krismas na Mwaka Mpya wahakikishe
wanakamilisja madeni yao.
“Hatutasita kumuondoa mtu yeyote atakayekuwa
akiendelea kudaiwa kwani atakuwa hana sifa za kupangisha katika majengo haya ya
viwanja vya ndege kwa kuanzia TBI na hapa TBII,” alisema Prof. Mbarawa.
Hatahivyo, aliyapongeza mashirika na ofisi
ambazo zimekuwa zikilipa kwa wakati fedha za pango, ambapo uaminifu huo
utawasaidia kupata nafasi katika jengo jipya la la tatu la abiria, ambalo
litakuwa linauwezo wa kuhudumia abiria milioni sita (6) kwa mwaka.
Pia amewataka wale wasiowaaminifu wachague
kulipa madeni ya pango au wanaodaiwa na serikali au kuondoka, ili kutoa nafasi
kwa Watanzania wengine ambao wanania ya dhati ya kufanya biashara na Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wasimamizi wakuu wa viwanja vya serikali.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard
Mayongela alisema tayari zabuni mbalimbali zimeshatangazwa na kuwataka wadau
waliowaaminifu kujitokeza kuwania na kupata nafasi ya kufanya shughuli zao
kwenye eneo la JNIA.
“Tumeshatangaza zabuni hizo na kama mhe.
Waziri alivyosema zitakuwa za uwazi zikishirikisha wataalamu na tunauhakika
watapatikana watu wenye mapenzi mema ya kufanya biashara na serikali” alisema
Bw. Mayongela.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa
alitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) na kuridhishwa na kasi ya ujenzi,
ambapo amewapongeza TAA, Tanroads na Kampuni ya ujenzi ya Kimataifa ya Uholanzi
(BAM).
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw. Mayongela,
alisema kukamilika kwa jengo hilo kutatoa fursa nyingi za biashara zikiwemo
uwekezaji katika hoteli, kumbi za mikutano, ofisi, migahawa, maduka makubwa ya
bidhaa mbalimbali, huduma za kifedha (benki) na karakana za ndege.
No comments:
Post a Comment