TIMU ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, imeivua
ubingwa wa Kombe la Chalenji Uganda Cranes baada ya kuifunga mabao 2-1 katika
mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Moi mjini Kisumu leo.
Zanzibar ambayo awali ilikuwa haipewi nafasi ya
kufanya vizuri, iliwavua ubingwa Uganda katika mchezo huo wa nusu fainali ya
pili na sasa itakutana na wenyeji Kenya katika mchezo huo wa fainali.
Hii ni mara ya pili kwa Zanzibar kucheza nusu fainali
baada ya mara ya kwanza kufikia hatua hiyo mwaka 1995, ambapo ilitwaa taji hilo
kwa mara ya kwanza.
Mchezaji wa Zanzibar, Abdul-Azziz Makame ndiye
aliyeifungia timu hiyo bao la kwanza katika dakika ya 22 kabla mfungaji
anayeogoza kwa kupachika mabao katika mashindano hayo, Derrick Nsibambi kuisawazishia
Uganda na kufikisha mabao manne dakika saba kabla ya mapumziko.
Mohammed Issa Juma ndiye aliyeihakikishia Zanzibar
Heroes kucheza fainali na kunusa ubingwa baada ya kufunga bao la ushindi kwa penalty baada ya dakika 57 na kuiwezesha
timu hiyo ya kisiwani kuweka historia ya ushindi mjini Kisumu.
Sasa sasa watacheza na wenyeji Harambee Stars – ambao
waliifunga Burundi kwa bao baada ya muda wa nyongeza katika nusu fainali ya
kwanza baada ya timu hiyo kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida na
kuongezewa dakika zingine 30 kwenye Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.
Fainali hiyo itapigwa Jumapili, ambapo mshindi
atapatikana.
The Cranes walimaliza wakiwa 10 uwanjani baada ya
mchezaji aliyeingia akitokea benchi, Joseph Nsubuga alipotolewa nje baada ya
kuonyeshwa kadi yekundu ya moja kwa moja katika dakika ya 55 baada ya kumchezea
vibaya Ahmada Ibrahim katika eneo la hatari.
“Huu ulikuwa mchezo mgumu dhidi ya mabingwa watetezi,
Namshukuru Mungu na wachezaji wangu kwa ushindi huu uliotupeleka katika fainali
ya Cecafa Challenge Cup. Tulistahili kushinda leo kutokana na jinsi
tulivyocheza.”
“Tunaiheshimu Kenya ambao ni wapinzani wetu wajao
katika fainali. Na hiyo haina maana kuwa tunawaogopa bkwa sababu tumekuja hapa
kushinda kikombe.” Alisema kocha wa Zanzibar Hemed Morocco.
No comments:
Post a Comment