Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa tamasha la kila mwaka la michezo na
Utamaduni la Karatu wameongeza zawadi kwa washindi watatu wa kwanza wa michezo
yote itakayoshindaniwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo Meta Petro,
bingwa wa mwaka huu wa mbio za kilometa 10 kwa wanaume ataondoka na kitita cha
sh 500,000 huku mshindi wa pili akipata sh 300,000 wakati watatu ataondoka na
sh 250,000.
Zawadi kama hizo pia zitatolewa kwa washindi wa
kwanza hadi watatu wa mbio za wanawake za kilometa tano, huku watoto wadogo,
ambao watashiriki mbio za kilometa 2.5, wenyewe mwaka huu mshindi wa kwanza,
ataondoka na sh 100,000 badala ya 50,000.
Mbali na riadha, pia zawadi kwa washindi wa mbio za
baiskeli ambazo zitawashindanisha wanaume katika umbali wa kilometa 60 na
wanawake 30, nao mwaka huu wameongezewa zawadi.
Mbali na mbio na baiskeli, pia tamasha hilo
linashirikisha mchezo wa soka, mpira wa wavu, kwaya pamoja na ngoma za
utamaduni na sarakasi.
Alisema kuwa tamasha la mwaka huu linatarajia kuvuta
washiriki wengi baada ya klabu kibao na wanariadha binafsi na wapanda baiskeli
kujisajili kwa wingi kwa ajili ya kushiriki michezo hiyo.
Baadhi ya klabu za riadha ambazo zimethibitisha
kushiriki tamasha hilo ni pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),ambayo itakuwa
na zaidi ya wanariadha 25, Magereza Arusha yenye anariadha 20, Jambo Athletics
Club, Ketra zote za Arusha, Lingwa ya Singida na Lyan ya Mbulu.
Mbali na riadha, Petro alizitaja klabu za baiskeli
zilizothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Lake Manyara Cycling Club ya
Manyara, Hakika ya Arusha , Klabu ya Baiskeli ya Magugu na Arusha Cycling Club kutoka
mkoani humo.
Mbali na riadha na baiskeli, tamasha hilo pia
litakuwa na mpira wa wavu pamoja na soka, ambazo fainali zake zitafanyika
Desemba 22 ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha tamasha hilo, ambalo linatarajia
kufungwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison
Mwakyembe.
Tamasha hilo ambalo huandaliwa na Filbert Bayi
Foundation (FBF) kwa kushirikiana na TOC, Chama cha Riadha Karatu na
kudhaminiwa na Olympic Solidarity,limekuwa chachu ya kuibua vipaji hasa katika mchezo
wa riadha.
No comments:
Post a Comment