Na Mwandishi Wetu
SHINDANO la kumsaka MR Tanzania 2017 litafanyika jijini Dar es Salaam Desemba 15 katika hoteli ya MayFair, imeelezwa.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kujenga Mwili Tanzania
(TBBF), Francis Mapugilo alisema jijini Dar es Salaam kuwa, maandalizi ya shindano
hilo yanaendelea vizuri na hadi sasa kuna washiriki 60, ambao watachujwa na
kubaki 30 watakaoingia kambini.
Akifafanua kuhusu kumpata Mr Tanzania 2017, Mapugilo
alisema kuwa Desemba 12 kutakuwa na shindano la kumsaka Fashion Icon, ambalo
litafanyika kwa Hussein Pamba Kali, ambalo washiriki watavaa nguo mbalimbali na
yule mwenye mwonekano mzuri atashinda.
Alisema siku inayofuata, kutakuwa na shindano la
kumsaka Mr Fit, ambapo washiriki watachuana katika mazoezi mbalimbali yakiwemo
kuchomoka kwa kasi, kupiga pushapu na mazoezi mengine.
Mapugilo alisema kuwa shindano jingine dogo
litafanyika Desemba 14, ambalo litakuwa kumsaka Mr Photojenic, ambalo
litafanyikia katika eneo la kuogelea la hoteli ya MayFair.
Alisema katika shindano hilo atatafutwa mshiriki
mwenye m uonekano mzuri katika picha, ambapo pia washiriki watatembea na kupozi
ili kupata picha nzuri,ambazo zitashindanishwa na kumpata mshindi.
Alisema yote hayo yatakamilishwa Desemba 15 kwa
shindano kubwa na mshiriki atakayekuwa maarufu zaidi ndiye atayeibuka Mr
Tanzania 2017 na kupata nafasi ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Shindano hilo, Nilesh Batt alisema
kuwa shindano hilo limeandaliwa vizuri
ili kuhakikisha mshindi wa ukweli anapatikana ambaye atawakilisha vizuri
Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya Mr Afrika pamoja na yale ya dunia
yatakayofanyika mwakani Nigeria na Uingereza.
No comments:
Post a Comment