Thursday, 14 December 2017
Wanariadha kibao wajitokeza mbio za Karatu 2017
WANARIADHA na klabu mbalimbali za riadha zimejitokeza kwa wingi
kuthibitisha kushiriki tamasha la 16 la Michezo na Utamadani la Karatu
litakalofanyika Desemba 23, imeelezwa.
Mratibu wa tamasha hilo linalofanyika kila mwaka mjini humo, Meta Petro
alisema leo kwa njia ya simu kuwa, wanariadha binafsi au klabu zimethibitisha
kushiriki tamasha hilo, ambalo litamalizikia katika viwanja vya Mazingira Bora
mjini Karatu.
Petro alitaja baadhi ya klabu za riadha zilizothibitisha kushiriki kuwa
ni pamoja na Magereza Arusha, ambayo itakuwa na wanariadha 20, Jeshi la Kujenga
Taifa, Jambo Athletics Club, Ketra zote za Arusha, Lingwa ya Singida na Lyan ya
Mbulu.
Mbali na riadha, Petro alizitaja klabu za baiskeli zilizothibitisha
kushiriki kuwa ni pamoja na Lake Manyara Cycling Club ya Manyara, Hakika ya
Arusha , Klabu ya Baiskeli ya Magugu na Arusha Cycling Club kutoka mkoani humo.
Mbali na riadha na baiskeli, tamasha hilo pia litakuwa na mpira wa wavu
pamoja na soka, ambazo fainali zake zitafanyika Desemba 22 ikiwa ni siku moja
kabla ya kilele cha tamasha hilo, ambalo litafungwa na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe.
Petro alisema kuwa pia kutakuwa na burudani za ngoma za utamaduni,
kwaya pamoja na maigizo na sarakasi vitakavyofanyika wakati wa ufungaji wa
tamasha hilo la kila mwaka.
Wanariadha watachuana katika mbio za kilometa 10 na tano kwa wanaume na
wanawake huku watoto wadogo wakichuana katika mbio za kilometa 2.5 wakati mbio
za baiskeli zitakuwa za kilometa 60 kwa wanaume wakati wanawake watapiga pedari
umbali wa kilometa 30.
Tamasha hilo ambalo huandaliwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) kwa
kushirikiana na TOC, Chama cha Riadha Karatu na kudhaminiwa na Olympic
Solidarity,limekuwa chachu ya kuibua vipaji hasa vya mchezo wa riadha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment