Saturday 9 December 2017

Mkutano Mkuu TOC kufanyika kesho Zanzibar

Na Mwandishi Wetu
MKUTANO Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) unafanyika kesho mjini hapa, imeelezwa.

Huo ni Mkutano Mkuu wa kawaida wa mwaka, lakini ni wa kwanza tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mjini Dodoma Desemba 18 mwaka jana.

Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alisema leo Jumamosi mjini hapa kuwa, tayari maandalizi ya mkutano huo yameshakamilika na wajumbe walianza kuwasili tangu jana kwa ajili ya mkutano huo utakaofanyikia katika Kituo cha Amani Welezo.

Alitaja baadhi ya ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo mkuu kuwa ni pamoja na mahudhurio, kuthibitisha ajenda, kuthibitisha na kupitisha Mkutano Mkuu wa Uchaguzi 2016, salamu za Rais, TOC.

Bayi alizitaja ajenda nyingine kuwa ni pamoja na taarifa ya shughuli za Kamati ya Utendaji ya TOC kwa mwaka huu na kupitia na kupitisha kalenda ya shughuli za TOC kwa mwaka 2018.


Nyingine ni taarifa ya Mhazini Mkuu kuhusu mahesabu yaliyokaguliwa 2016, kupokea na kupitisha rasimi ua bajeti ya TOC kwa mwaka 2018 na mengineyo kwa ruhusa ya mwenyekiti wa Mkutano Mkuu.

No comments:

Post a Comment