Tuesday, 19 December 2017

Kocha, Wakala wa Gatlin katika Kashfa ya doping

NEW YORK, Marekani
BINGWA wa dunia wa mbio fupi Justin Gatlin (pichani) anasema kuwa `ameshtushwa na kushangazwa’ na madai ya dawa za kuongeza nguvu zilizotolewa dhidi ya kocha na wakala wake.

Viongozi wa riadha na Taasisi ya Kupambana na Dawa za Kuongeza Nguvu Michezoni wameanza uchunguzi kile ambacho Rais wa mchezo huo duniani ameyaita  ‘madai mazito’ kuhusu Dennis Mitchell na Robert Wagner.

Gazeti la The Daily Telegraph liliandika Wagner – wakala anayehusiana na Gatlin – alitoa dawa hizo zilizopigwa marufuku kwa waandishi wa habari ambao hawakujulikana.

Mkanda wa video uliotolewa na Telegraph unamuonesha mtu ambaye gazeti hilo limesema ni Wagner alimshauri Gatlin kutumia dawa hizo zilizopigwa marufuku, kama vile wanariadha wengine wa mbio fupi wa Marekani.

Gazeti hilo limesema kuwa kocha wa Gatlin, ambaye ni bingwa wa medali ya dhahabu wa Olimpiki Mitchell, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanariadha wanaweza kukwepa kubainika kutumia dawa hizo kwa sababu vipimo vinashindwa kubaini dawa hizo walizotumia.

WOTE WAKANA TUHUMA
Akiandika katika Instagram jana, Gatlin alisema kuwa “atamtimua mara moja” Mitchell "mara nitakapobaini ukweli kuhusu tuhuma hizi ".

Mwanariadha huyo Mmarekani mwenye umri wa miaka 35 alisema “hatumii na hajawahi kutumia” dawa hizo za kusisimua misuli.

Aliongeza: "Suala hilo tayari ameanza kulishughulikia kisheria ili kuhakikisha hakuna watu wengine wanatoa taarifa za uongo kama hizi kuhusu mimi.”

The Telegraph limesema waandishi wa habari ndio walimpeleka wawakilishi wa kampuni ya filamu, ambaye alijifanya kama kocha amabaye anamfundisha kocha mwanariadha wake kuwa nyota.

Taasisi mbalimbali ikiwemo Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) pamoja na Chama cha Maadili, na Taasisi ya Kuzuia Matumizi ya Dawa za Kuongeza Nguvu ya Marekani (Usada) zilisema zimeanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo.

Rais wa IAAF Lord Coe alisema: "Tuhuma hizi ni kubwa sana na ninajua Kamati Huru ya Maadili ya Riadha itachunguza kwa kina kuhusu tuhuma hizo…”


Gatlin, ambaye alitumikia mara mbili vifungo baada ya kubainika kutuia dawa hizo, alishinda medali ya dhahabu katika mbio za meta 100 katika mashindano ya riadha ya Dunia mwezi Agosti jijini London, akimshinda Usain Bolt katika mchezo wa mwisho wa meta 100 kwa Mjamaica huyo kabla hajastaafu kucheza mbio.

No comments:

Post a Comment