Na Mwandishi Wetu
MABONDIA wa timu ya taifa ya Tanzania wamesema kuwa
wanataka kupatiwa kambi ya kudumu pamoja na vifaa ili waweze kujiandaa vizuri
kwa ajili ya Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Aprili mwakani Gold
Coast, Australia.
Kocha Mkuu wa timu hiyo inayoendelea na mazoezi
kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, Said Omary au maarufu kama Gogopoa alisema
juzi kuwa timu inaendelea na mazoezi lakini ina changamoto kibao.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na
mabondia kukosa vifaa vya mazoezi zikiwemo padi, glovu na vifaa vingine pamoja
na kutokuwa katika kambi ya kudumu na hivyo kushindwa kufuatilia mazoezi
vizuri.
Amesema anaiomba Serikali kuingia kati suala hilo ili
timu hiyo ipate mahitaji yake na iweze kujiandaa vizuri kwa ajili ya michezo
hiyo ya mwakani.
Naye nahodha wa timu hiyo, Seleman Kidunda alisema
kuwa mabondia wanahitaji kambi ya kudumu ili kuwapunguzia gharama za kwenda na
kurudi kutoka mazoezini.
Alisema mbali na nauli, mabondia hawana fedha za
kupata mlo baada ya mazoezi na timu hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa
vya mazoezi,
Pia Kidunda amesema kuwa pia mabondia wanahitaji
mechi za majaribio ili kuwaweka fiti na kuwapatia uzoefu kwa ajili ya
mashindano ya kimataifa.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT) zinaendelea baada
ya simu ya katibu mkuu wake, Makore Mashaga kuitwa bila kupokelewa leo.
No comments:
Post a Comment