Bi. Delfine Mulogo wakati wa uhai wake. |
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),
inamlilia kwa masikitiko makubwa Mwanasheria wake Bi. Delfine Mulogo
(32) aliyekuwa Kituo cha kazi cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA) aliyefariki dunia Desemba 25.
Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Bw.
Mtengela Hanga akisoma wasifu wa marehemu katika kanisa Katoliki Parokia ya
Mtakatifu Augustine Mbezi Temboni, alisema, atakumbukwa kwa uchapakazi, uhodari
na uadilifu wake kazini.
“Tunasikitika kumpoteza mwanasheria huyu kijana,
kwa niaba ya Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, tunatoa
pole kwa wafiwa kwa kuondokewa na mpendwa wao, lakini sisi kama mamlaka na
taifa kwa ujumla tumempoteza mtu muhimu sana aliyekuwa mchapakazi, tutamkumbuka
sana marehemu,” alisema Bw. Hanga.
Marehemu ambaye ameacha mume Bw. Alex Temba
na watoto wawili, Faith (9) na Harieth (4) alihamishiwa TAA tarehe
01/04/2016 akitokea Halmashauri ya Manispaa ya mji wa Songea alipokuwa akifanya
kazi kama mwanasheria kuanzia mwaka 2012.
Naye Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria
Tanzania (TLS), Bw. Stephen Msechu alisema marehemu alikuwa mwanachama tangu
alipoapishwa kuwa Wakili mwaka 2012 na kupewa namba ya uanachama 3361 na
amekuwa akishirikiana nao katika shughuli mbalimbali kwa uadilifu mkubwa.
Hata hivyo, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia
ya Mtakatifu Augustine lililopo Mbezi Temboni, Padri Fidelis Mfaranyembo
aliwataka waombolezaji waliofika kuuaga mwili wa marehemu Delfine kujiandaa wakati wote kwa kuwa hawajui siku wala saa watakayotwaliwa.
Padri Mfaranyembo alisema pia waombolezaji
wahakikishe wanakuwa watu wa sala wakati wote ili kumuombea marehemu aweze
kupokelewa na aingie katika ufalme wa mbinguni, kwani ufalme huo upo kwa kuwa
kunamaisha baada ya kifo.
“Kuna mwanafalsafa mmoja wa zamani, Plato
alitafakari sana kuwa mwanadamu akifa
anakwenda wapi? na akaona kila mwanadamu anabeba roho ya muumbaji na hivyo unapokufa roho inarudi kwa yule
aliyeiumba, "alisema na kuongeza:
" Plato anatufundisha ya kwamba mwisho wa maisha yake hapa duniani
Mwanadamu anarudi kwa Mungu wake kulingana na namna alivyokuwa akiishi na
wengine hapa duniani,” alisema Padri Mfaranyembo.
Pia amemtaka mume wa marehemu Bw. Temba
asifadhaike kwa kuondokewa na mkewe, bali ajikabidhi kwa Mungu kwa kumuomba
hakika atamsaidia kwa kumtia nguvu na kumpa uwezo wa kuendelea kuwahudumia
watoto wake kwa kadri ya uweza wake Mungu.
Marehemu alipata elimu ya msingi katika shule
ya Oysterbay (1991), baadaye sekondari ya St. Mathew (1998), na baadaye elimu
ya Kidato cha Tano na Sita katika shule ya Wasichana ya Kibosho (2004), na
mwaka 2008 alihitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha
Tumaini.
Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa Jina Lake Lihimidiwe. Amina.
No comments:
Post a Comment