Friday 10 February 2017

YANGA YAWAACHA NGOMA, BOSSOU NA WENGINE SAFARI YA COMORO



Na Waandishi Wetu
MSHAMBULIAJI tegemeo wa Yanga, Donald Dombo Ngoma atakosekana katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Ngaya Club de Mde nchini Comoro Jumapili.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina ameteua wachezaji 20 kwa safari ya kesho Alfajiri kwenda Comoro na Ngoma atakosekana kwa sababu ni majeruhi baada ya kuumia katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Stand United Ijumaa iliyopita, Yanga iksihinda 4-0 naye akifunga bao moja.

Pamoja na Ngoma, wengine watakaokosekana kwenye safari hiyo ni kipa Benno Kakolanya, mabeki Mtogo Vincent Bossou, Pato Ngonyani, Andrew Vincent ‘Dante’ na washambuliaji Malimi Busungu, Matheo Anthony.Lwandamina amewaacha Kakolanya, Matheo, Bossou na Ngonyani kwa sababu hawamo katika programu zake za mchezo huo, wakati Dante anatumia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mechi ya mwisho ya Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe mjini Lubumbashi, DRC Agosti, mwaka jana – na Busungu mgonjwa.

Wachezaji watakaoondoka na Yanga kwa usafiri wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC) Alfajiri ya kesho ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’. 

Mabeki ni Juma Abdul, Hassan Kessy, Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondani, 

Viungo ni Deus Kaseke, Haruna Niyonzima, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Saidi Juma ‘Makapu’, Juma Mahadhi, Yusuph Mhilu, Obrey Chirwa, Justine Zulu  na Emmanuel Martin wakati mshambuliaji ni Amissi Tambwe pekee.

Benchi la ufundi litaongozwa na Kocha Mkuu; George Lwandamina, Kocha wa Viungo, Noel Mwandila wote Wazambia, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa Makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Daktari Edward Bavu, Watunza Vifaa, Mohamed Omary Mwaliga na mchua misuli Jacob Sospeter Onyango.

Msafara huo utakuwa chini ya mwakilishi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mussa Mohammed Kisoki na Paul Malume wa Yanga.

Ikiwasili, Yanga kesho itapata fursa kufanya mazoezi yake pekee kwenye Uwanja utakaochezewa mchezo wa Jumapili.

Mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 18 na mshindi atakutana na Zanaco ya Zambia katika Raundi ya Kwanza.

No comments:

Post a Comment