Wednesday 1 February 2017

MBOMA AIONYA GHANA KUTOIDHARAU CAMEROON NUSU FAINALI AFCON KESHO


Mashabiki wa Cameroon wakishangilia katika moja ya mechi za timu yao.

LIBRAVILLE, Gabon
MCHEZAJI bora wazamani wa mwaka wa Afrika, Patrick Mboma, ameionya Ghana kutoidharau Cameroon katika mchezo wao wa nusu fainali utakaofanyika kesho Alhamisi.

Mboma  ni mchezaji wazamani wa kimataifa wa Cameroon aliyeichezea nchi hiyo kwa mafanikio makubwa.
Mchezaji huyo bora wa Afrika wa mwaka 2000 anasema kuwa Ghana inapewa nafasi kubwa ya kucheza fainali ya mashindano hayo kutoka na uzoefu na kiwango cha wachezaji wake.

Lakini mchezaji huyo aliigeukia timu hiyo na kuitaka kutoidharau hata kidogo Cameroon ambayo inaweza kuwa tatizo kubwa kwa Black Stars.

Mboma alisema, “Nina furaha kuona timu ya Cameroon yenye kujiamini na zaidi, yenye mawazo mazuri katika nusu fainali ya mashindano haya, na hata kama timu hiyo ilikuwa haitarajiwi kufika hapo.”

Timu hiyo ya Cameroon sio miongoni mwa timu zilizokuwa zikipewa nafasi ya kufanya vizuri kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

Cameroon iliifunga Senegal iliyokuwa ikipewa nafasi ya kufanya vizuri na sasa Cameroon wamo katika mbio za ubingwa.

Mpambano huo wa leo utakaofanyika Franceville utakuwa ni mrudiano wa nusu fainali ya Afcon wa mwaka 2008 Afcon, ambako Cameroon iliifunga Ghana kwa bao 1-0 jijini Accra na kucheza fainali yao ya mwisho ya mashindano hayo.

Zote Ghana na Cameroon kila moja imetwaa mara nne taji la Afcon, ambapo kila moja anataka kuongeza idadi hiyo ya mataji.

No comments:

Post a Comment