Friday 24 February 2017

Mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza kuziamua Simba na Yanga taifa kesho Jumamosi


Na Mwandishi Wetu
MWAMUZI Mathew Akrama wa Mwanza ndiye rasmi atakayeamua mchezo wa maasimu wa jadi wa Simba na Yanga Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kufuatia kikao cha juzi jioni cha Kamati ya Waamuzi kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Akrama ameteuliwa kuamua mchezo huo utakaofanyika kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mwamuzi huyo atasaidiwa na washika vibendera, Mohammed Mkono wa Tanga na Hassan Zani wa Arusha. Mchezo huo ni wa marudiano baada ya ule wa duru la kwanza kuzikutanisha timu hizo na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

Katika mchezo huo wa kwanza, Yanga bao lake lilifungwa na Amissi Tambwe Oktoba 1, imeweka kambi Kigamboni, Dar es Salaam, wakati Simba iliyosawazisha kupitia kwa Shiza Kichuya ilikuwa visiwani Zanzibar.

Hii ni mara ya pili kwa Akrama kuchezesha mechi ya watani, baada ya Oktoba 3, 2012 kuchezesha mechi ya Ligi Kuu pia timu hizo zikitoka sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa. 

Katika mchezo huo ulioanza Saa 1:02 usiku, Akrama alimtoa kwa kadi nyekundu winga Simon Msuva wa Yanga dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu beki wa Simba, Juma Nyosso.

Siku hiyo, Simba walitangulia kwa bao la kiungo Amri Kiemba katika dakika ya pili, kabla ya mshambuliaji Said Bahanuzi kuisawazishia Yanga dakika ya 63 baada ya beki Paul Ngalema kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Lakini Akrama alilaumiwa kwa kumuonesha kadi ya njano badala ya nyekundu kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ licha ya kumchezea rafu mbaya beki wa Yanga, Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake ikachukuliwa na Juma Abdul.

Na pia alilaumiwa kuwa kutomchukulia hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana kupoteza muda tangu mwanzo, na alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.

Haikuwa ajabu Oktoba 6 Akrama alipoondolewa kwenye orodha ya wamuzi wa kuchezeaha Ligi Kuu baada ya kuvurunda mechi hiyo namba 80, huku aliyekuwa mshika kibendera namba mbili, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam akipewa onyo.

Wapenzi wa soka wanatakiwa kuwa na subira ili kuona nini kitatokeakatika mchezo huo uliosubiriwa kwa muda mrefu na kutawaliwa na tambo kutoka kwa wapenzi wa soka hapa nchini.

No comments:

Post a Comment