Wednesday, 8 February 2017

MTANZANIA Davids Bwana ameshika nafasi ya pili katika shindano la insha kwa wanafunzi la DStv Eutelsat Star



Na Mwandishi Wetu
MTANZANIA Davids Bwana ameshika nafasi ya pili katika shindano la insha kwa wanafunzi la DStv Eutelsat Star za mwaka huu.

Muethiopia Leoul Mesfin ndiye aliyeshika nafasi ya kwanza katika shindano hilo lilofanyikia Lagos, Nigeria jana.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mawasiliano wa Multchoice- Tanzania, Johnson Mshana, kwa upande wa bango, Emmanuel Ochenje wa Nigeria ndiye kinara akifuatiwa na Aobakwe Letamo wa Botswana.

Tuzo hizi ambazo zimeshirikisha wanafunzi zaidi ya 1,000 kutoka mataifa 20 barani Afrika, ziliandaliwa na Multichoice Afrika kwa kushirikiana na Shirika la Mambo ya Anga la Eutelsat na zenye lengo la kukuza vipaji vya kiakili kwa watoto.

Alisema kuwa kwa nchi za Afrika Mashariki Bwana wa Tanzania ndiye pekee aliyefanya vizuri katika shindano hilo lenye lengo la kuleta mageuzi yenye tija katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

Moja ya vigezo vikubwa kwa mshiriki kushinda ni kiwango cha juu cha usahihi alichoandika, ubunifu wa kisayansi, uhalisia wa alichokiandika na dhana ya ugunduzi aliyoijenga kwenye andiko au bango lake. 

Dhana ya mwaka huu imelenga kuwajengea wanafunzi mtazamo wa umuhimu wa setelaiti kwa maendeleo ya teknolojia barani Afrika.
Mesfin anapata fursa adhimu ya kufanya ziara nchini Ufaransa katika jiji maarufu la Paris na kutembelea kituo kikubwa cha anga cha Eutelsat na pia fursa ya kwenda kushuhudia  urushwaji wa setelaiti angani.

Wakati Bwana naye atapata fursa ya kwenda Afrika Kusini kutembelea ofisi za Multichoice pamoja na Idara ya Anga ya Afrika Kusini akiwa kama mgeni maalum wa Multichoice.

Shule walikotoka washindi wote wanne zitapata zawadi ya kufungiwa ving’amuzi vya DStv pamoja na kifurushi maalum cha Elimu.

Akizungumza juu ya matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande alisema wamefurahishwa sana na matokeo hayo na huu ni uthibitisho tosha kuwa Watanzania wana uwezo mkubwa wa kushindana na kushinda katika anga za kimataifa.

 “Sisi Multichoice Tanzania tunasema Ni Zamu Yetu! Ni zamu yetu watanzania kuwika kila mahali duniani, kwani uwezo huo tunao na sasa ari hiyo pia tunayo, “alisema.

Akizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa mkuu wa jopo la watahini wa tuzo hizo Claudie Haigneré, mwanamama mwenye sifa na ujuzi mkubwa katika elimu ya anga aliyewahi kuwa Waziri nchini Ufaransa na sasa ni Mshauri maalum wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Masuala ya Anga la Ulaya (European Space Agency - ESA).

Alisema: “kushiriki kwangu kwenye tuzo hizi kwa mara ya kwanza kumenipa mwangaza mwingine hususan kwakuwa mada ya mwaka huu ilikuwa yenye kutoa changamoto kubwa. 

Mitazamo na mawazo yaliyotolewa na washiriki kuhusiana na hatma ya sayansi ya setelaiti yameonesha bayana ni jinsi gani kizazi kipya cha wanasayansi wa Afrika kilivyo na uchu na ari kubwa ya kuleta mbapinduzi makubwa katika sekta hiyo kwa manufaa ya bara la Afrika. 

Sisi watahiniwa tulijikita kwenye mjadala mzito ili kuhakikisha tunamtunuku ushindi Yule hasa anayestahili.”

Akizungumza kwa Furaha kubwa juu ya matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema wamefurahishwa sana na matokeo hayo na huu ni uthibitisho tosha kuwa watanzania wana uwezo mkubwa wa kushindana na kushinda katika anga za kimataifa. “Sisi Multichoice Tanzania tunasema Ni Zamu Yetu!

 Ni zamu yetu watanzania kuwika kila mahali duniani kwani uwezo huo tunao na sasa ari hiyo pia tunayo. Kitendo cha kijana huyu kuibuka miongoni mwa washindi katika mashindano yanayohusisha kazi bora kabisa kutika mataifa 20 kote barani Afika ni heshima kubwa sana kwetu sote” alisema Maharage na kuongeza kuwa hii itawatia sana moyo wanafunzi wa Tanzania na hivyo kuongeza jitihada na bila shaka mwakani washindi wa kwanza kwa pande zote watatokea Tanzania.

Pamoja na mwanamama Claudie Haigneré, Wengine walioshiriki kwenye jopo hilo la watahini ni pamoja na  Mtanzania Jenerali Ulimwengu, Msomi mwanasheria na nguli wa Habari hapa nchini; Ronke Bello, Afisa Mtendaji Mkuu wa Innovative Technology Literacy Services Ltd (Nigeria); Rodney Benn, Mkurugenzi wa Kanda (Africa) wa shirika la Eutelsat na  Melt Loubser, Meneja Mkuu wa Teknolojia ya Matangazo kutoka MultiChoice Africa. Wengine ni Elizabeth Ohene Muandishi wa habari ambaye aliwahi kuwa Waziri nchini Ghana; Prof. Stephen Simukanga,  aliyekua Kansela wa Chuo Kikuu cha Zambia ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Elimu ya Juu nchini Zambia  na John Ugbe, Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Nigeria.

No comments:

Post a Comment