Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Simba jana ilifanya kweli baada ya kuibuka na ushindi mzito wa
mabao 3-0 dhidi ya Majimaji ya Songea katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara
uliofanyika mjini hapa.
Kwa ushindi huo, wekundu hao wa Msimbazi wamebakisha pointi moja kuifikia
Yanga iliyopo katika nafasi ya kwanza kwa kuwa na pointi 49.
Simba ilianza mbio za ushindi katika dakika ya 20 kwa bao lililofungwa na
Kichuya.
Wakati wa mapumziko kulitokea tafrani kati ya makomandoo wa Simba na
Yanga aliyekaa jukwaani juu, ambapo alitakiwa kuondoka haraka kwani yeye sio
mgeni rasmi.
Bao la pili la Simba lilifungwa na Said Ndemla huku lile la tatu kupitia
kwa Mrundi Laudit Mavugo.
Kocha wa Simba Joseph Omog alifanya mabadiliko katika mchezo huo, ambao
mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa ruvu, Dk Binilith Mahenge baada ya kuwatoa
Jamal Mnyate na kumuingiza Pastory Athanas.
Kocha wa Majimaji, Kally Ongala baada ya mchezo huo aliwalaumu wachezaji
wake kwa kucheza chini ya kiwango, ambapo alisema kipigo hicho ni cha
kujitakia.
Alisema wachezaji wake walishindwa kufuata maelekezo tofauti na
walivyocheza dhidi ya Ndanda ya Mtwara na kusababisha kupoteza mchezo huo.
Naye Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja aliwapongeza wachezaji wake
kwa ushindi huo, ambapo alisema wamecheza vizuri kwa kufuata maelekezo.
Mayanja aliwaahidi wapenzi wa Simba kuwa makosa ya nyuma hayatajirudia
katika mechi zijazo, ambapo sasa ni mwendo mdundo na wataendelea kushinda kila
mechi zijazo.
Wakati huohuo, Azam FC leo inaikaribisha Ndanda FC katika mchezo mwingine
utakaofanyika kwenye Uwanja wa Chamazi Mbagala jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment