Friday, 3 February 2017

YANGA YAITISHA SIMBA KWA KUICHAPA STAND UNITED MABAO 4-0 UWANJA WA TAIFA



Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Tanzania Bara Yanga leo walizidi kujichimbia kileleni baada ya kuichapa Stand United ya Shinyanga kwa mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo ni mkwara mzito kwa Simba katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo baada ya wiki iliyopita kuwatoa kileleni. Wekundu hao wa Msimbazi leo wanacheza na Majimaji ya Songea katika mchezo utakaofanyika ugenini.

Yanga imefikisha pointi 49 ikiwa ni pointi nne zaidi ya Simba, ambayo leo itacheza na Majimaji ya Songea na hata ikishinda itakuwa nyuma kwa pointi moja.

Yanga katika mchezo huo walipata bao la kuongoza katika dakika ya 19 lililofungwa na Doland Ngoma kwa kichwa akiunganisha wavuni mpira wa Simon Msuva.

Baada ya kushindwa kufunga katika dakika ya 11, Msuva alisahihisha makosa yake katika dakika ya 27 pale alipoifungia timu yake bao la pili baada ya krosi ya Ngoma.

Stand United ambao katika mchezo wa kwanza dhidi ya mabingwa hao wa Tanzania Bara Yanga walishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, nusura wafunge katika dakika ya 26 wakati Jacob Massawe aliposhindwa kuutumbukiza mpira wavuni akiwa nje ya 18.

Dakika ya 38, Stand walikosa tena bao baada ya Seleman Selembe kuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini alipiga mpira uliopanguliwa kifundi na kipa wa Yanga Munish aliyeupangua kabla ya kuudaka.

Yanga waliakianza kipindi cha pili kwa bao lililofungwa na Chirwa huku Msuva akikosa penalti katika dakika ya 58 baada ya kupaisha mpira.

Penalti hiyo ilitolewa baada ya Revocatus Richard kufanya madhambi ndani ya 18, lakini Msuva alipiga shuti lililopa juu ya lango.

Mkongwe Nadir Haroub alifunga bao la nne kwa Yanga katika dakika ya 68 kwa kichwa akiunganisha wavuni kona iliyochongwa na Juma Abdul.

Vikosi vilikuwa:-
Yanga:Deogratius Munis, Nadir Haroub, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani/Vicend Andrew, Justine Zulu, Simon Msuva, Thabiti Kamusoko, Donald Ngoma, Obrey Chilwa na Haruna Niyonzima/Emmanuel Martin.

Stand United: Sebastiane Stanley/Mohamed Makaka, Jacob Massawe, Erick Mulilo, Adeyum Ahmed, Revocatus  Richard, Ibrahim Job, Abdulaziz Makame, Adam Salamba/Kheri Rashid, Frank Khamis, Absalim Chidiebele na Seleman Selembe.

No comments:

Post a Comment