Thursday 9 February 2017

Tanzania yaendelea kuporomoka viwango vya soka duniani, Cameroon yapanda kinoma



Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imezidi kuporomoka katika orodha ya viwango vya ubora wa soka duniani na sasa inashika nafasi ya 158 kutoka 156 iliyoshika Januari.

Kwa mujibu wa viwango hivyo vilivyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) jana, Tanzania imepata pointi 152 na kujikuta katika nafasi hiyo.

Hiyo inatokana na timu ya taifa, Taifa Stars kutocheza mechi yoyote ya kimataifa tangu Desemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa viwango hivyo, Uganda bado inaongoza kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ikiwa nafasi ya 75.

Hata hivyo, timu hiyo imeporomoka kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya 73 mwezi uliopita baada ya kuishia hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) iliyomalizika Gabon wiki iliyopita. Kenya inashika nafasi ya pili kwa ukanda wa Shiriisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ikiwa nafasi ya 87 ikifungana na wenyeji wa Afcon 2017 Gabon.

Katika nchi nyingine za ukanda wa Cecafa, Rwanda ipo nafasi ya 100, Ethiopia ni ya 103, Burundi ya 138, Sudan 139, Sudan Kusini ya 169, Djibouti, Eritrea na Somalia zikifungana katika nafasi ya 205.

Mabingwa wapya wa Afrika, Cameroon wamepanda kwa nafasi 29 hadi ya 33, huku washindi wa pili Misri wamerudi juu hadi nafasi ya 23 baada ya kuporomoka miaka miwili iliyopita.

Kwa ujumla, Argentina imeendelea kuongoza kwa ubora wa soka duniani, wakifuatiwa na mahasimu wao, Brazil nafasi ya pili na Ujerumani wakishika nmafasi ya tatu.

No comments:

Post a Comment