Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda amejitoa mhanga kwa kuagiza kuswekwa ndani kwa askari Polisi zaidi ya
tisa wa mkoa huo pamoja na kuwataka wasanii maarufu nchini akiwamo aliyewahi
kuwa Miss Tanzania, Wema Sepetu kujisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi,
akiwatuhumu kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Mbali na Wema ambaye alikuwa Miss
Tanzania 2006 na kwa sasa ni mwigizaji maarufu, Makonda akawataka wasanii
wengine maarufu kujisalimisha leo katika kituo hicho jijini Dar es
Salaam, wakiwemo Khaleed Mohamed (TID),
Winfrida Josephat (Recho), Khery Sameer (Mr Blue), Hamidu Chambuso (Dogo
Hamidu) na Rashid Makwiro (Chid Benz).
Makonda anakuwa kiongozi wa kwanza nchini
kujitokeza hadharani na kutaja wahusika au watuhumiwa wa biashara ya dawa za
kulevya kwa majina, baada ya miaka mingi wanasiasa kuishia kueleza kuwa wanayo
majina ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu yenye fedha nyingi, lakini hawakuyataja hadharani.
Katika mkutano wake na waandishi wa
habari jana, Makonda aliwataja askari hao kwa jina moja moja ambao ni Swai,
Neri, Willy, Mkomeo wote wa Kituo cha Polisi Oysterbay, aliyekuwa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, Inspekta Fadhil wa Kinondoni,
Steven wa Kinondoni, James wa Kinondoni, CP Dotto wa Kituo cha Kijitonyama na
WP Glory wa Kituo cha Kawe.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Mkuu wa mkoa huyo pia amewataka wamiliki
wenye leseni za kuendesha sehemu za starehe ambazo zinasadikika kujihusisha na
uuzaji wa dawa hizo, kujisalimisha leo saa tano katika Kituo Kikuu cha Polisi
wakiwemo wamiliki wa George Dragon, Element na Cuba Bar.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa pili kushoto) akishiriki katika mbio za pole pole au jogging Temeke jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mrisho Mpoto au Mjomba. |
Makonda ambaye kabla ya uteuzi wake
aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, aliwaambia waandishi wa habari kwamba
amefikia hatua hiyo baada ya kufanya msako wa kuwakamata wahusika wa dawa za
kulevya katika mkoa huo na baadhi ya wananchi kuwataja askari hao kuwa
wanahusika kuwaficha wauzaji wa dawa hizo.
Alisema baada ya msako, wananchi walikuwa
wanawataja wahusika wa dawa hizo, lakini polisi hawawajui ndipo alipopata
taarifa kuwa wanashirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, jambo
linalofanya kushindwa kutokomeza dawa hizo katika mkoa huo.
“Kwa mamlaka niliyonayo nataka wakamatwe
kama wapo ndani ya mkoa au nje waletwe na wawekwe mahabusu pale Central, watoe
maelezo kwa nini wananchi wanawataja, kuna wengine wanatajwa kuwapigia simu
wahusika wakati wakienda kuwakamata na wanatumiwa hela kupitia simu zao, hizi
ni tuhuma na wao wana nafasi ya kujieleza,” alisema Makonda.
Aidha, Makonda aliwataja baadhi ya watu
wanaosadikika kuwa ni wafanyabiashara wa dawa hizo ambao tayari wameshakamatwa
akiwemo Ahmed Ngahemela (Pettit man), Said Lina maarufu kama Alteza, Nassoro
Nassoro, Bakari Khelef pamoja na Omary.
“Wapo wengi, lakini hawa ndio tayari
tumewakamata na wengine wamekutwa na dawa hizo, tunaendelea na msako ambao
nitauendesha mimi mwenyewe nikishirikiana na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama, lengo ni kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya katika mkoa huu
(Dar es Salaam) inatokomezwa,” alifafanua Makonda.
Makonda pia ametoa siku saba kutokomezwa
kwa vijiwe na maeneo yote yanayojihusisha na uuzaji dawa za kulevya katika mkoa
huo.
Kamanda-Jeshi-la-Polisi-Kanda-Maalum-ya-Dar-es-Salaam-Simon-Siro. |
“Mnafahamu nipo na Kamishna Sirro na
kamati yake baada ya siku saba nitawaambia kama watashindwa kutokomeza dawa za
kulevya Dar es Salaam maana yake wamekosa sifa za kuendelea kuwa askari katika
mkoa wetu, kwa kuwa wameshindwa kuwafahamu wauzaji,” alibainisha Makonda.
Naye Kamanda Sirro alisema atalizungumzia
hilo kwa waandishi wa habari atakapokutana nao leo.
No comments:
Post a Comment