Thursday 9 February 2017

Mashindano netiboli Afrika Mashariki kuanza Nairobi, Kenya Aprili 23



Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Annie Kibira

Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya netiboli ya Afrika Mashariki yatafanyika jijini Nairobi, Kenya kuanzia Aprili 23 hadi 30, imeelezwa.

Tanzania katika mashindano hayo itawakilishwa na Uhamiaji, JKT pamoja na Jeshi Stars, ambao ni washindi wa kwanza hadi watatu wa Ligi Daraja la Kwanza.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Annie Kibira amesema kuwa, baada ya kimya kirefu hatimaye juzi wametangaziwa tarehe ya mashindano hayo.

Kibira aliwataka wawakilishi hao kuanza maandalizi mapema ili kuhakikisha mwaka huu wanmarudi na taji hilo, ambalo kwa muda mrefu hawalijawahi kuja nchini.

“Nawaomba wawakiishi wetu waanze mapema maandalizi ili waweze kufanya vizuri na kutwaa taji, ambalo kwa muda mrefu halijawahi kuja nchini, “alisema Kibira.
Alisema mara nyingi timu zetu zimekuwa zikiishia katika nafasi ya pili na kuendelea, ambapo alitoa wito akitaka zijiandae mapema ili kwenda kushindana badala ya kushiriki.

Kwa upande wa Zanzibar timu zitakazowakilisha ni pamoja na Mafunzo, JKU na Zima Moto, ambazo tayari zimeanza maandalizi kwa ajili ya mashindano hayo.

Hatahivyo, timu za Zanzibar zimekuwa hazifanyi vizuri katika mashindano hayo, ambayo Kenya na Uganda ndio zimekuwa zikiwika kila mwaka

No comments:

Post a Comment