Thursday, 9 February 2017

Wabunge waipiga jeki Serengeti boys ili ifanye vizuri Afcon 2017



Nahodha wa Serengeti Boys Issa Makame (kulia) akipokea mchango wa Sh 800,000/= kutoka kwa Wabunge Ester Bulaya aliyetoa Sh 300,000 na Mbunge Almas Maige mjini Dodoma jana baada ya vijana hao kutembelea Bunge kwa Mwaliko maalum wa Spika wa Bunge. (Na Mpigapicha Wetu).

Na Waandishi Wetu
WABUNGE  wamepanga kuichangia timu ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys sehemu ya posho yao ya vikao vya jana.

Serengeti Boys iliyotembelea Bunge kwa mwaliko maalumu baada ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana wa umri huo zilizopangwa kufanyika Gabon, Mei mwaka huu.

Timu hiyo ilipata nafasi hiyo baada ya kushinda rufaa iliyoikata kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupinga Congo Brazzaville kumchezesha mchezaji aliyezidi umri. 

 Spika wa Bunge Job Ndugai alisema wabunge wote waliohudhuria kikao cha jana watakatwa Sh 220,000 kwenye posho yake ili kuichangia timu hiyo.

Awali,  hoja hiyo ililetwa na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema). 

Bulaya aliomba mwongozo wa Spika akitaka wabunge hao waichangie timu hiyo kupitia posho zao za siku moja.

Kwa mujibu wa Bulaya, timu hiyo inahitaji kwa sasa mchango wa hali na mali kutoka kwa Watanzania wote kwa kuwa inatarajia kwenda kushiriki michuano hiyo ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa timu ya vijana ya Tanzania kupata nafasi hiyo. 

“Taifa letu, wabunge, wananchi kwa ujumla wanapenda michezo, vijana wetu hawa wamefuzu katika mataifa ya Afrika na kama tulivyosikia bajeti yao ni Sh bilioni moja, naomba mwongozo wako mheshimiwa Spika, na sisi wabunge tuichangie,” alisema.
 
 Hata hivyo, kabla Bulaya kumaliza hoja yake ya kuomba mwongozo ili wabunge waruhusiwe kukatwa posho yao ya siku moja kwa ajili ya kuiunga mkono timu hiyo, Bunge hilo lililipuka kwa kelele za kuunga mkono hoja hiyo, ingawa wapo wengine walioikataa.

Awali, Spika wa Bunge Ndugai alipoitambulisha mbele ya wabunge hao timu hiyo na kuimwagia sifa kwa kufuzu kuiwakilisha Tanzania, wabunge wote waliishangilia kwa kugonga meza lakini hali ilibadilika pale suala la kuichangia lilipofika.

 Kutokana na kelele hizo Spika Ndugai alimruhusu Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), naye atoe hoja yake kuhusu suala hilo ambapo aliunga mkono na kuwataka wabunge wawe wazalendo.

 “Uganda timu yao ilipoenda kucheza michuano ya kombe la Afrika, wabunge wake waliichangia timu yao na sisi tutoe jamani,” alisema Keissy.

 Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa vikali na Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF), ambaye alisema suala la michango linaendana na hiari ya mtu hivyo kwa wabunge wanaotaka kuichangia timu hiyo waichangie na wasiotaka waachwe.

“Hili Bunge lisitumike sehemu ya michango kwa kila kitu, sasa katika hili anayetaka achange asiyetaka aachwe,” alisisitiza.

 Wakati wote huo, kelele zilishamiri kwa wabunge kugonga meza kila upande ukiunga mkono hoja yake.

Katika kuhitimisha suala hilo, Spika Ndugai alisema ili kupata muafaka wa suala hilo, ni vyema Bunge hilo likatumia uratibu wa kibunge wa kuamua jambo ambalo lina mgawanyiko mkubwa.

Hata hivyo, alisema timu hiyo inapaswa kuungwa mkono na watanzania wote na wabunge ndio wanapaswa kuonesha mfano kutokana na heshima kubwa timu hiyo iliyoliletea taifa.

Kiongozi huyo wa Bunge, alihoji Bunge hilo na kuwataka wale wanaoukubali wabunge wachangie posho ya Sh 220,000 timu hiyo waseme ndio na wanaopinga waseme hapana.

 Hata baada ya kuhoji sauti za waliosema ndio na hapana almanusura zilingane lakini Spika huyo alimtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kusimamia suala hilo na fedha hizo ziwasilishwe kwa timu hiyo.

Baadaye akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema kwa mujibu wa utaratibu mchango huo utakatwa kwa wabunge wote waliohudhuria siku hiyo. Alisema, idadi kamili ya wabunge watakaochangia ataifahamu leo maana kuna wabunge wengine huingia bungeni jioni na hivyo kushindwa kufahamu idadi kamili ya watakaochangia kwa jana. 

Hata hivyo baada ya kutoka nje kwa picha ya pamoja na timu hiyo, Bulaya na  Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almas Maige walichanga Sh 800,000 taslimu na kuwapatia wachezaji hao.

Timu hiyo ilifika bungeni hapo ikiwa imeongozana na viongozi mbalimbali wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya rais wake, Jamal Malinzi.

No comments:

Post a Comment