Na Mwandishi Wetu
VILIO, majonzi na simanzi vilitawala jana katika kijiji cha Mbweera,
Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wakati wa mazishi ya Mwandishi wa gazeti la
Habarileo, Arnold Swai (28) anayetajwa kuwa ni "Nyota iliyong'aa na
kuzimika ghafla".
Swai aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM, (UVCCM) wilayani
Hai alifikwa na mauti jumapili iliyopita katika ajali ya gari iliyotokea katika
eneo la Mwika, Moshi vijijini na kusababisha vifo vya watu wanane.
Kwa mujibu wa gazeti la leo la Habarileo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliongoza umati wa waombolezaji
waliofika kuuga mwili wa Swai katika kanisa la Kiinjili Kilutheri (KKKT)
usharika wa Masama kati na kuzikwa kijijini kwao.
Kinana alisema, Swai alikuwa na maono makubwa na kama asingefariki
angekuwa kijana ambaye angeshika nafasi mbalimbali za uongozi na angetoa
mchango kwa taifa na kwa taaluma yake.
"Mungu ametuleta duniani na atatutoa kwa muda wake, lakini ameweka
siri ya siku ya kutuondoa ndiyo maana tunahuzunika. Tuwe watu wema wenye
huruma, tumkumbuke Mungu na kuwasaidia wengine, Arnold alitimiza hilo".
Alisema
Akizungumza katika ibada, Mchungaji Andrew Munisi aliwataka vijana kuacha
kujihusisha na dawa za kulevya na kunywa pombe badala yake wafanye kazi na
kuiga mfano wa Swai ambaye alikuwa kijana mwenye maono na muwajibikaji.
Baadhi ya waandishi wa habari waliofanyakazi na Swai walisema, ingawa
alikuwa mwanasiasa, lakini alitofautisha muda wake wa kufanya siasa na kazi
zake kitaaluma.
Msiba huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wa CCM,
akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Mkuu wa Mkoa
wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, Kamanda wa Polisi Mkoa, Wilbroad Mutafungwa,
Mwenyekiti wa CCM mkoa, Iddy Juma, viongozi mbalimbali wa UVCCM, wakuu wa
wilaya na madiwani.
Swai alifikwa na mauti ajalini wakati akitoka kwenye maadhimisho ya miaka
40 ya kuzaliwa kwa CCM, ambayo kimkoa yalifanyika Rombo, katika tarafa tano kwa
kufanya mikutano ya ndani.
No comments:
Post a Comment