Na Mwandishi Wetu
MSHINDI wa pili wa shindano la insha la DStv Eutelsat 2017, Davids Bwana
jana alikabidhiwa rasmi cheti chake kutoka kwa MultiChoice-Africa.
Bwana ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya wavulana ya
Feza, alikabidhiwa cheti hicho shuleni hapo jana na meneja masoko wa
MultiChoice-Tanzania, Alpha Mria mbele ya waalimu, baadhi ya wanafunzi na mama
yake mzazi, Dk Esther Mbutolwe.
Davids Bwana akiwa na mama yake mzazi, Dk Esther Mbotolwe mara baada ya kijana huyo kukabidhiwa cheti chake jana. |
Baada ya kukabidhiwa cheti hicho, Bwana alisema anamshukuru Mungu kwa
kumsaidia kupata nafasi hiyo ya pili kutokana na jitihada kubwa alizofanya.
Alisema haikuwa rahisi kupata nafasi hiyo kwani kulikuwa na changamoto
nyingi kutoka kwa washindani wenzake, ambao baadhi yao walimkatisha tamaa kuwa
hawezi kushinda.
Bwana ameshika nafasi ya pili katika uandishi wa insha nyuma ya
Muethiopia, Leoul Mesfin huku Tanzania ikiwa nchi pekee ya Afrika Mashariki
iliyoshika nafasi ya juu.
Kwa ushindi huo, Bwana atapata fursa kufanya ziara nchini Afrika Kusini
kutembelea ofisi za MultiChoice pamoja na Shirika la Anga la Afrika Kusini.
Katika shindano hilo, mwanafunzi alitakiwa kuandika insha inayoeleza
elimu ya anga, hasa masuala ya satelaiti na jinsi ambavyo ingeweza kulisaidia
bara la Afrika.
Mkurugenzi wa shule za Feza, Ibrahim Rashid (kulia) akiwa na Bwana. |
MultiChoice-Tanzania kupitia meneja masoko wake ilisema kuwa
imefurahishwa na ushindi huo na itaendelea kuwashindanisha wanafunzi katika
mashindano mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa shule za Feza, Ibrahim Rashid alisema wamefurahishwa
na ushindi huo kwani Bwana ameongeza tuzo za kimataifa katika kabati la shule
hiyo.
Alisema shule hiyo ilikuwa na tuzo 19 za kimataifa na baada ya ushindi wa
mwanafunzi huyo, sasa zimefikia 20.
Naye mama wa mwanafunzi huyo, aliwataka wazazi wenzake kuwapa fursa
watoto wao ili waweze kuonesha vipaji vyao badala ya kuwabana.
Alisema wazazi wanatakiwa kuwa karibu na watoto wao na kuwasaidia katika
ukuaji wao kitaaluma kwani huo ndio urithi mzuri kuliko kitu kingine.
Congratulations Davids
ReplyDelete