Wednesday, 28 March 2018

Uchukuzi Sports Waiva Kwa Mei Mosi 2018

Kocha Kingsley Marwilo (katikati) jana akisimamia mazoezi ya timu ya soka ya Uchukuzi yanayofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Airwing, wakijiandaa na mashindano ya Kombe la Mei Mosi yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Aprili 16, 2018.

Na Bahati Mollel,TAA
TIMU za michezo mbalimbali za Uchukuzi SC zimeiva kutokana na mazoezi zinazofanya kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Airwing, kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mei Mosi yatakayoanza Aprili 17 hadi Mei 1 kwenye viwanja mbalimbali Jijini Arusha,

Kocha Mkuu wa timu ya soka, Zeno Mputa amesema wachezaji wake wameiva na wapo tayari kwa mashindano ya Mei Mosi, kutokana na kuripoti kwa wingi na kufanya mazoezi kwa bidii.
Wachezaji wa timu ya kamba ya Wanawake ya Uchukuzi wakifanya mazoezi kwa kuvutana na timu ya wanaume (haionekani pichani) wakijiandaa na mashindano ya kombe la Mei Mosi yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Aprili 16, 2018.
Mputa amesema amewapima wachezaji wake kwa kuwapa mazoezi magumu kwa siku tatu mfululizo, lakini wote waliweza kufika kwenye mazoezi kwa siku zilizofuata.

“Yale mazoezi magumu ni kama copper test na nilifanya hivyo nikiwa na lengo la kupima utimilifu wa mwili, na wamefuzu wote kutokana na kuendelea na mazoezi, siku zilivyofuata tofauti na awali nilidhani watakuwa wamechoka na kushindwa kufanya mazoezi tena,” amesema Mputa.
Hata hivyo, anasema tayari wameshacheza mechi moja ya kirafiki na timu ya Kipunguni na kutoa sare ya bao 1-1, lakini wanategemea mechi nyingine mbili zitakazochezwa baadaye wiki hii ili kujiweka imara zaidi.

Naye kocha wa timu ya kamba kwa wanawake na wanaume, Abunu Issa amesema wachezaji wake wamekuwa wakiripoti mazoezi kila siku na kufanya mazoezi makali, ikiwemo kuvuta kamba wenyewe kwa wenyewe.
Daktari Hawa Senkoro (kushoto) wa timu ya Uchukuzi akimchua misuli mchezaji wa kamba wa wanaume Augustino Saqware baada ya kubanwa na misuli wakati wa mazoezi yanayoendelea kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Airwing ya kujiandaa na michuano ya Mei Mosi itakayofanyika Arusha kuanzia Aprili 16, 2018.
“Timu zangu hizi zimekuwa zikijituma hivyo naamini pia tutafanya vizuri katika mashindano, kwani nimekuwa nikiwapima kila baada ya mazoezi kwa wanawake kuvutana na wanaume na kiwango chao ni kizuri,” amesema Abunu.

Kwa upande wa riadha, Kocha wake Kingsley Marwilo amejihakikishia wachezaji wake kufanya vyema kutokana na mazoezi wanayofanya, yakiwemo ya kujijengea misuli ikiwa ni kufanya mazoezi na wachezaji wa soka.

Timu ya netiboli, inayofundishwa na Kocha Judith Ilunda nayo imeendelea na mazoezi kwenye viwanja vya Bandari Kurasini, ambapo sasa wanacheza na timu za Zanzibar zinazoshiriki tamasha la Pasaka linalofanyika kwa kupokezana na  Tanzania Bara.


 Kipa Paul Chiwangu (kushoto) akijiandaa kudaka mpira wa krosi uliopigwa na Godwin Ponda wakati wa mazoezi yanayofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Airwing ya kujiandaa na mashindano ya Mei Mosi yatakayofanyika kuanzia Aprili 16 hadi Mei Mosi katika viwanja mbalimbali Jijini Arusha.


Uchukuzi SC ndio mabingwa watetezi kwenye michezo ya kuvuta kamba kwa wanaume na wanawake, wakati kwa netiboli walitwaa ushindi wa pili sawa na karata, bao, draft na baiskeli  wanawake, huku katika soka walishika nafai ya tatu.     
Aziza Tamim (kushoto) akimtazama mpinzani wake Stumai Mbato (kulia) wakati wakifanya mazoezi ya kucheza karata kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Airwing wanapojiandaa na michuano ya Mei Mosi  itakayofanyika Arusha kuanzia Aprili 16, 2018. Kwanza kushoto ni Sharifa Amiri anayecheza bao akiwaangalia.    
 
Mweka Hazina wa timu ya Uchukuzi, Bw. Benjamin Bikulamti akitoka kununua maji ya wachezaji wa michezo mbalimbali waliokuwa wakifanya mazoezi kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Airwing kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Mei Mosi yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Aprili 16, 2018.

No comments:

Post a Comment