Sunday, 25 March 2018

Kamati ya Bunge Yataka TAA Kutafuta Hati Miliki za Viwanja vya Ndege Kuepuka Migogoro na Wananchi

Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Mhe. Godftey Mgimwa (aliyekunja mikono) akifuatia kwa makini maelezowakati Kamati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) ilipotembelea Kiwanja cha Ndege cha Songwe jana.

Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), imeiomba Serikali kuangalia upya na kuviondoa vikwazo vinavyoizuia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kupata hati miliki ya viwanja vyote vya ndege nchini, ili kuepuka migogoro na wananchi wanaovamia maeneo hayo mara kwa mara.

Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Stephen  Ngonyani ‘ Prof. Majimarefu’ ametoa kauli hiyo wakati kamati hiyo ilipofanya ziara kwenye Kiwanja cha Ndege cha Songwe, ambapo ameiomba serikali kulegeza vikwazo vilivyopo ili TAA iweze kupata hati miliki za viwanja vyote inavyosimamia.

“Mimi naomba mahali penye vikwazo vinavyokwamisha hizi hati kupatikana, basi vilegezwe na wapewe hati,” amesema Mhe. Ngonyani.  
Mjuumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Pwani, Mhe, Zainabu Vulu (kushoto) akisikiliza jambo, wakati kamati hiyo ilipotembelea Kiwanja cha Ndege cha Songwe. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), Mhandisi Prof. Ninatubu Lema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dr. Raphael Chegeni amesema kati ya viwanja 58 vinavyomilikiwa na serikali ni nane pekee vyenye hati na vingine kutokuwa na hati hizo.

“Naiagiza Bodi ya Ushauri ya TAA kushirikiana na ofisi au Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili hati zipatikane, ambazo zitasaidia kuweka kumbukumbu nzuri ya mali za serikali,” amesema Dr. Chegeni.

Hatahivyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw.  Richard Mayongela amesema kuwa vikwazo vikubwa ni wananchi waliovamia maeneo ya viwanja vya ndege, pamoja na vingine kuwa na matamko ya serikali yenye kuonesha uhalali na yanayozuia mtu mwingine kuingilia maeneo hayo kwa kufanya makazi au shughuli nyingine yeyote, bado yamekuwa kikivamiwa.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), wakipata maelezo mbalimbali kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Raphael Chegeni (hayupo pichani) walipofanya ziara kwenye Kiwanja cha Ndege cha Songwe, jana.
“Wananchi wamekuwa wakivamia maeneo ya viwanja vya ndege tena yakiwa yanamatamko rasmi ya serikali, na hata wengine wanavamia mara baada ya tamko kutolewa, hii ndio migogoro mikubwa,” amesema Bw. Mayongela.

Aidha Kamati hiyo ya PIC, pia imegundua kusuasua kwa ujenzi wa jengo la abiria, ambapo wameagiza likamilike haraka. Jengo hilo likikamilika linatarajia kuhudumia abirai 500,000 kwa mwaka.
 Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Joachim Maambo (wakwanza kulia nyuma) akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi na Matengenezo, Mhandisi Mbila Mdemu wakiandika vitu mbalimbali, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) ilipotembelea Kiwanja cha Ndege cha Songwe. 
Viwanja vya ndege vimekuwa vikitoa mchango mkubwa katika kuimarisha usafiri wa anga nchini, ambapo vimekuwa vikijengwa na kukarabatiwa mara kwa mara ili kuiweka miundombinu hiyo katika hali nzuri.

No comments:

Post a Comment