Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) aliyefungiwa
maisha na Kamati ya Maadili, Michael Wambura ameibuka na kulaani uteuzi wa
Kamati ya Utendaji kumteua Athumani Nyamlani kukaimu nafasi hiyo.
Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, juzi ilimteua Nyamlani
kukaimu nafasi hiyo, huku ikimthibitisha Kidao Wilfred kuwa Katibu Mkuu katika
kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Wambura katika taarifa hiyo kupitia mwanasheria wake, Emmanuel
Muga alisema kuwa anapinga uteuzi huo wa Nyamlani kuchukua nafasi yake wakati
rufaa yake aliyokata bado haijasikilizwa na kutolewa uamuzi.
Taarifa hiyo ya kurasa moja inaeleza kuwa Kamati ya Utendaji Machi
24, 2018 iliendesha zoezi la uteuzi lisilo halali na kuvunja ibara namba 34 (1)
ya Katiba ya TFF, ambayo inaeleza kuwa nguvu ya kumchagua na kumuondoa makamu
wa rais ni ya Mkutano Mkuu.
Pia Wambura ameshtushwa na kitendo cha kuwabadilisha baadhi ya
wajumbe wa Kamati ya Rufaa, ambapo uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji sio wa haki
na unaopigana na ibara ya 34 (2) ya Katiba ya TFF.
Ibara hiyo inasomeka: “Chombo hicho huru cha kisheria cha TFF
wajumbe wake hawaruhusiwi kuondolewa kabla ya kipindi chao bila ya kuidhinishwa
na Mkutano Mkuu.
Nyamlani anachukua nafasi ya Wambura aliyefungiwa maisha na Kamati
ya Maadili kutojihusisha na masuala ya mpira, na Kidao alikuwa akikaimu nafasi
hiyo takribani miezi nane sasa.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao cha Kamati ya Utendaji, ambacho
kilikutana kwenye hoteli ya Sea Scape zinasema, Nyamlani amepata sifa za
kukaimu nafasi hiyo kwa sababu kanuni na taratibu za TFF zinatamka kuwa nafasi
za kuchaguliwa mjumbe atakaye kaimu awe mjumbe wa Kamati ya Utendaji aliyedumu
kwa kipindi kirefu.
“Kanuni zinamtaka mjumbe wa muda mrefu ambaye yupo kwenye Kamati
ya Utendaji, na ukiangalia kwa sasa wajumbe ambao wana muda mrefu ni Nyamlani,
Ahmed Mgoyi na Khalid wa Tanga ila sasa Nyamlani ndio amewazidi wote, hivyo
kamati ilimkaimisha yeye hadi uchaguzi mdogo utakapotangazwa,” kilisema chanzo
hicho.
Hata hivyo, kazi ya kumwidhinisha Nyamlani kukaimu nafasi hiyo
haikuwa rahisi kwani ililazimika kupigwa kura ili kumpitisha, ambapo zile za
ndio zilikuwa nyingi, hivyo akapitishwa mpaka pale mkutano mkuu wa TFF
utakavyoamua vinginevyo.
Nyamlani ambaye alikuwa makamu wa Rais kipindi cha uongozi wa
Leodgar Tenga, aliingia kwenye Kamati ya
Utendaji kwa kuteuliwa na Rais Wallace Karia yeye na Ahmed Mgoyi.
Kidao alikuwa akikaimu nafasi ya ukatibu mkuu baada ya yule wa
awali, Selestine Mwesigwa, yeye na Malinzi kushtakiwa kwa madai ya ubadhilifu
na makosa mengine.
No comments:
Post a Comment