Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa
Ngorongoro Marathon 2018 wametangaza zawadi, ambapo mshindi wa kwanza ataondoka
na kitita cha Sh milioni 1, ambazo zitafanyika Aprili 21.
Mkurugenzi wa mbio
hizo, Meta Petro (pichani chini), akizungumza kwa njia ya simu kutoka Karatu, Arusha jana
alisema kuwa, mshindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake, kila mmoja ataondoka
na Sh milioni 1.
Alisema kuwa mshindi
wa pili atapewa Sh 500,000, huku mshindi wa tatu kwa kila upande ataondoka na
Sh 250,000.
Alisema kuwa pia
kutakuwa na mbio za kujifurahisha za kilometa tano pamoja na zile za watoto
wadogo za kilometa 2.5, ambazo hazina viingilio ili kuwawezesha watoto
kujitokeza kwa wingi.
Alisema lengo la
mbio za mwaka huu ni Kukimbiza Jangili, ambapo wanapiga vita mauaji ya wanyama
kama vile tembo, simba, chui, twiga na wengine, ambao wamekuwa wakiuawa kwa
sababu ya pembe, meno, kucha na ngozi zao.
Alisema wanyama kama
tembo na faru wamekuwa wakiuawa kwa ajili ya biashara haramu ya pembe zao huku
twiga na pundamilia wakiuawa kwa ajili ya nyama, na simba na chui wamekuwa
wakiuawa kwa ajili ya ngozi zao.
Akielezea ada ya
ushiriki, Petro alisema kuwa kwa Watanzania watakaokimbia kilometa 21 watalipa
Sh 10,000 kwa fomu huku wageni watalipa dola za Marekani 50.
Alisema kwa wale
watakaoshiriki kilometa tano kama timu, kuanzia mtu mmoja hadi watano,
watalipia dola za Marekani 500, wakati mtu mmoja mmoja Mtanzania atalipia Sh
10,000 na asiye Mtanzania atalipa dola 10.
Wakati huohuo, Petro amesema kuwa bado wanasaka wadhamini
kwa ajili ya mbio hizo, ambazo mbali na kupiga vita vya ujangili, pia
zinatangaza vivutio vya utalii nchini.
No comments:
Post a Comment