Na Mwandishi Wetu
MECHI ya watani
wa jadi Simba na Yanga ambayo ilikuwa ichezwe Aprili 7 kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam sasa itachezwa Aprili 29.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPBL),
Boniface Wambura alisema wamefanya mabadiliko ya ratiba kwa mechi kadhaa kwa
sababu wanataka Ligi Kuu imalizika Mei 26 kama ilivyopangwa.
"Ratiba
imebana sana hivyo mchezo wa kiporo wa Njombe na Simba utachezwa Aprili 3 na
tumefanya kazi ya ziada kukubaliana na Njombe kwani wanasema ratiba siyo rafiki
kwao lakini nashukuru wametuelewa," alisema Wambura.
Pia Wambura
alisema mchezo wa Simba na Yanga utachezwa Aprili 29 badala ya Aprili 7 ili
kuipa Yanga nafasi kujiandaa na mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya
Wolayta Dicha ya Ethiopita unaotarajiwa kuchezwa Aprili 4 kwenye uwanja wa
Taifa.
Mechi ya Simba
na Yanga inatarajiwa kuwa ya vuta nikuvute hasa kwa vile timu hizo zimeonesha
upinzani mkubwa kileleni mwa msimamo na hivyo mpaka sasa yeyote kati yake
anaweza kuwa bingwa.
Simba inaongoza
msimamo kwa uwiano mzuri wa mabao baada ya kulingana pointi 46 na Yanga iliyo
nafasi ya pili.
Wambura alisema
ratiba hiyo inaweza kufanyiwa tena marekebisho endapo Yanga itafuzu kwenye
hatua ya makundi huku akisema sababu nyingine zinazofanya ratiba kupanguliwa ni
kutokana na timu kutokuwa na viwanja vyao hivyo wamiliki wa viwanja wanapokuwa
na shughuli za kijamii mechi zinasogezwa mbele.
Mechi nyingine
zilizofanyiwa marekebisho ni Mbao dhidi ya Lipuli utakaochezwa Aprili 6 na
tarehe hiyo tena Mwadui Shinyanga.
Mtibwa Sugar
itacheza na Simba Aprili 9 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Yanga itacheza na
Stand United Aprili 11, Simba itaivaa Mbeya City Aprili 12 na Aprili 16
itaikaribisha tena Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Taifa.
Lipuli itakuwa
mwenyeji wa Simba Aprili 20 na Majimaji itacheza na Ruvu Shooting Aprili 28.
Wambura alisema
wamepata kibali cha kutumia uwanja wa Taifa kwa michezo inayohusu Simba na
Yanga isipokuwa mchezo wa Yanga dhidi ya Azam FC utalazimika kuchezwa kwenye
uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment