Monday, 26 March 2018

‘Brazil Nzuri Lakini Bado Inamuhitaji Neymar’


MUNICH, Ujerumani
BRAZIL ni moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika fainali za Kombe la Dunia 2018, lakini kuumia kwa nyota Neymar bado kunaidhoofisha timu hiyo, anasema winga wa Ujerumani Leroy Sane.

Sane pia ni kiungo wa vinara wa Ligi Kuu ya England, Manchester City.

"Brazil haimtegemei Neymar kama ilivyokuwa mwaka 2014," alisema winga wa Manchester City Sane.

"Wako katika nafasi nzuri na wana wachezaji nyota wachache wapya, lakini bado inafanya tofauti Neymar awepo au asiwepo.

Ujerumani itaikaribisha Brazil katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaofanyika leo Jumanne kwenye Uwanja wa Olimpiki mjini Berlin, ikiwa ni sehemu ya kuipa mazoezi timu hiyo kwa ajili ya Kombe la Dunia Juni nchini Urusi.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza tangu Ujerumani ilipoifunga Brazil kwa mabao matano ndani ya nusu saa wakati ikishinda 7-1 katika nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014.

Katika mchezo huo, mshambuliaji wa Brazil Neymar alikuwa nje kutokana na maumivu. Mchezaji huyo ghali kabisa duniani anauguza jeraha lake baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu.

Anatarajia kuwa fiti kwa wakati kwa ajili ya Kombe la Dunia, ambalo litaanza Juni 14.

Brazil iliifunga Urusi mabao 3-0 Ijumaa katika mchezo mwingine wa kimataifa wa kirafiki, huku mabao matatu yakifungwa na Miranda, Paulinho na Philippe Countinho aliyefunga kwa penalti katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Moscow wa Luzhniki, ambao utaandaa fainali ya Kombe la Dunia Julai 15.

Ujerumani ilijipima nguvu kwa kutoka sare ya 1-1 na Hispania huko Duesseldorf wakati bao la mapema la Rodrigo Moreno kwa wenyeji lililofuta lile la Thomas Mueller la kipindi cha kwanza.

Kocha Mkuu wa Ujerumani, Joachim Loew alisema kuwa kipigo cha mabao 7-1 kitadumu kwa miaka 10, 20 au 30 ijayo kila timu hizo zitakapokutana.

Loew alisema kuwa anatarajia kufanya mabadiliko matano kutoka katika timu iliyotoka sare na Hispania.

Mueller na Mesut Ozil wamepewa mapumziko na Loew, wakati kiungo wa Liverpool Emre Can ameachwa kutokana na maumivu ya mgongo.

No comments:

Post a Comment