Monday, 23 January 2017

Ligi ya Mabingwa wa Afrika yasogeza mbele mechi ya Simba na Yanga sasa kuzipiga februari 25



Na Mwandishi Wetu
MCHEZO wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya mahasimu, Simba na Yanga umesogezwa mbele hadi Februari 25, badala ya Februari 18, mwaka huu, imeelezwa.
 
Habari kutoka ndani ya Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema kwamba sababu ya kusogezwa mbele kwa mchezo huo ni muingiliano na ratiba ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
 
Kwa mujibu wa ratiba hiyo ya Afrika, Februari 10, mwaka huu, Yanga watakuwa wageni wa Ngaya FC katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Mde mjini Mde nchini Comoro, kabla ya kurudiana Februari 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa sababu hiyo, mchezo wa Simba na Yanga usingeweza kufanyika tena Februari 18 na busara za TFF zimeupeleka hadi Februari 25.

Baada ya kusimama mwishoni mwa wiki iliyopita, mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zinatarajia kuendelea tena katika viwanja tofauti huku Simba ikiendelea kung'ara kileleni na kupumuliwa kwa karibu na Yanga wakitofautiana kwa pointi mbili tu.


No comments:

Post a Comment