MCHEZAJI
na kocha wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Charles Boniface Mkwasa (Pichani) leo ametambulishwa rasmi
kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, akichukua nafasi ya Baraka Deusdedit anayerejea
kwenye Idara yake ya Fedha.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari leo katika Makao Makuu ya klabu hiyo, Jangwani, Dar es
Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba Mkwasa anaanza
majukumu yake rasmi Februari 1, mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga akizungumza leo na waandishi wa habari. |
“Na
hii si mara ya kwanza, hata Zambia, Kalusha Bwalya amewahi kuwa Katibu Mkuu wa
Chama cha Soka nchini humu huku wakijua kuwa ni mchezaji mstaafu au kocha,
Yanga tumemuona Mkwasa ni bora katika nafasi hiyo,” alisema Sanga.
Mkwasa
alishukuru kushika nafasi hiyo na kuahidi kuifikisha Yanga katika malengo
yaliyowekwa. “Naomba nieleweke wazi kuwa mimi ni Katibu Mkuu wa Yanga na wala
siyo kocha, najua kuna watu watafikiria kuwa narejea kwa mlango wa nyuma, kamwe
sitaingilia masuala yoyote ya ufundi zaidi ya kufanya yale yaliyomo katika
majukumu yangu,” alisema Mkwasa.
“Ninaomba
ushirikiano kutoka kwa wanachama, mashabiki, viongozi wenzangu, sisi sote tupo
hapa Yanga kwa ajili ya kuiletea maendeleo na si vinginevyo,” alisema.
Mkwasa anarejea Yanga ndani ya mwezi mmoja tangu aondolewe timu ya taifa ya
Tanzania, Taifa Stars na nafasi yake kupewa Salum Mayanga.
No comments:
Post a Comment