Na Mwandishi Wetu
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF), limetoa nafasi
ya mwisho kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Jamhuri ya Congo (FECOFOOT)
kumpeleka mchezaji Langa Lesse Bercy jijini Libreville, Gabon kwa ajili ya
kipimo kipya cha MRI ili kutambua umri wake.
CAF limetaka FECOFOOT kumpeleka mchezaji huyo huko Libreville, Gabon
ndani ya siku 10 zijazo kuanzia jana Januari 12, 2017.
CAF limepata kumwita mchezaji huyo mara mbili mwaka jana, na FECOFOOT
imeshindwa kumpeleka kwa sababu mbalimbali wanazozijua FECOFOOT.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya kimataifa ya vijana wenye umri wa
chini ya miaka 17, vijana waliohitajika kucheza ni wale wenye umri wa chini ya
miaka 17.
Langa Lesse Bercy, amelalamikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kwamba amezidi umri hivyo kuhitajika kumpeleka kwani hakustahili kucheza
hatua ya kufuzu kwa michuano hiyo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.
Fainali za vijana zinatarajiwa kufanyika katika nchi nyingine
itakayotangazwa hapo baadaye baada ya Madagascar kuondolewa kuandaa fainali
hizo baada ya kubainika kutokamilisha baadhi ya taratibu.
Hii inatokana na ripoti ambayo CAF wameipata kutoka kwa wakaguzi wa
maandalizi ya fainali hizo. CAF imefungua kandarasi ya kwa nchi wanachama
wengine kuandaa fainali hizo. Mwisho wa kupokea maombi ni Januari 30, mwaka
huu.
Kadhalika Kamati ya Utendaji ya CAF, imemteua Rais wa zamani wa TFF,
Leodegar Chilla Tenga kuwania nafasi ya uwakilishi katika Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Katika nafasi hiyo kutoka nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza, Tenga
atachuana na Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Zambia, Kalusha
Bwalya na Kwesi Nyantakyi wa Ghana.
Wengine waliopitishwa kuwania nafasi ya uwakilishi katika Kamati ya
Utendaji ya FIFA kutoka nchi za Afrika ni Tarek Bouchamaoui wa Tunisia ambaye
anaingia kwenye kundi la nchi zinazozungumza lugha za Kiarabu, Kireno na
Kihispaniola.
Kwa nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa wamo Constant Omari Selemani
wa DR Congo na Augustin Sidy Diallo wa Cote d’Ivoire wakati nafasi nyingine za
wazi ihuhusisha mwanamke mmoja, wamo Almamy Kabele Camara (Guinea), Chabur Goc
(South Sudan), Danny Jordaan (Afrika Kusini), Hani Abo Rida (Misri) na Lydia
Nsekera (Burundi).
No comments:
Post a Comment