ISTAMBULI, Uturuki
KWA uchache watu 39, wakiwemo wageni 16, wamekufa
katika shambulizi lililofanyika katika klabu ya usiku jijini hapa. Waziri wa
Mambo ya Ndani wa Uturuki amesema.
Suleyman Soylu pia alibainisha kuwa, Polisi bado wanawasaka “magaidi” hao waliofanya
shambulizi hilo katika klabu hiyo ya usiku ya Reina kwa saa 7:30 usiku kwa saa
za hapa.
Hatahivyo, kwa saa kadhaa baada ya shambulio hilo,
mamlaka za taifa zilikuwa kimya kuhusu suala hilo.
Watu wengine 69 walipatiwa matibabu hospitalini,
alisema waziri huyo.
"Usakaji wa magaidi hao bado unaendelea…Natarajia
(washambuliaji) watakamatwa haraka kwa mapenzi ya Mungu, “ alisema Soylu.
Mamlaka ya Uturuki imevizuia vyombo vya habari
kuripoti shambulio hilo, lakini alizuii taarifa za viongozi.
Gavana wa Jiji la Istanbul, Vasip Sahin awali alibainisha
kuwa ofisa wa polisi alikufa katika shambulio hilo.
Pia mshambuliaji mmoja alihusi, alisema gavana huyo,
wakati Kituo cha Televisheni cha CNN cha Uturuki kiliripoti kuwa, mshambuliaji
huyo alivalia vazi la Father Krismas .
"Magaigi wakiwa na silaha…walifanya vitendo vya
kikatili ikiwemo kuwafyatulia risasi raia wema na watu wengine waliokuwa
wakisheherekea Mwaka Mpya na kucheza, “alisema
Sahin alipozungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio katika eneo la Ortakoy.
Klabu hiyo sio maarufu tu kwa Waturuki, bali pia hata
kwa wageni kutoka nje ya nchi, ambao walipenda kwenda kula bata, kwa mujibu wa
Mtangazaji wa Shirika la Utangazji la Uingereza la BBC, Selin Girit jijini Istanbul.
Aliongeza kuwa watu walioshuhudia tukio hilo walisema
kuwa washambuliaji walikuwa wawili.
Iliripotiwa kuwa ndani ya klabu hiyo ya usiku
kulikuwa na watu zaidi ya 700 wakati shambulio hilo likitokea, ambapo baadhi
yao walirukia katika maji ili kujiokoa.
Shirika la Habari la Dogan liliriopit kuwa baadhi ya
mashuhuda walidai kuwa baadhi ya washambuliaji hao walikuwa “wakizungumza Kiarabu”
wakati channeli ya Televisheni ya Uturuki ya NTV ilisema polisi maalum walikuwa
wakipekuwa klabu hiyo ya usiku.
Rais wa Marekani Barack Obama, ambaye yuko katika
mapumziko huko Hawaii, ni miongoni mwa viongozi wa kwanza wa kimataifa kutoa
taarifa baada ya kutaarifiwa na timu yake.
"Rais ametuma salamu za rambirambi kwa kupotea
kwa maisha ya watu wasio na hatia…”ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Obama
iliyotolewa na msemaji wa Ikulu ya Marekani Eric Schultz.
Serikali ya Uturiki imetoa amri ya kuzuia kwa muda
vyombo vya habari vya hapa kuripoti taarifa hizo, kutokana na suala la
kiusalama.
Hii sio mara ya kwanza kwa amri kama hiyo kutolewa.
Istanbul ilikuwa katika hali ya taadhari huku kukiwa
na askari polisi zaidi ya 17,000 wakiwa kazini jijini hapa, kufuatia kuwepo na
matukio kadhaa ya kivamizi katika miezi ya hivi karibuni.
Vitendo vingi vya kigaidi vimekuwa vikifanywa na Dola
ya Kiislamu (IS) na wale wanaofahamika kama askari wa Kikurdi.
Chini ya wiki mbili, Balozi wa Urusi nchini hapa, Andrei Karlov, aliuawa kwa kupigwa risasi na
askari wa Uturuki ambaye hakuwa kazini Mevlut Mert Altintas wakati akihutubia
katika jiji la Ankara mwezi uliopita.
Baada ya mauaji hayo muuaji alikuwa akipiga kelele
kuwa kitendo hicho ni kulipa kisasi kwa Urusi kujiingiza katika mgogoro katika
jiji la Syria la Aleppo.
Mashambulizi
makubwa Uturuki kwa mwaka 2016
Desemba
10:
Mashambulizi mawili ya mabomu yalifanyika nje ya uwanja wa soka jijini Istanbul
na kuua watu 44, kundi la askari wa Kikurdi walidai kuhusika ba tukio hilo.
Agosti
20:
Shambulizi la bomu katika sherehe ya harusi huko Gaziantep liliua watu 30, huku
kundi la IS likihisiwa kuhusika.
Julai
30:
Wapiganaji 35 wa Kikurdi walijaribu kuvamia ngome ya kijeshi na kujikuta
wakiuawa na Jeshi la Uturuki.
Juni
28:
Shambulio la risasi na bomu katika uwanja wa ndege wa Ataturk jijini Istanbul viliua
watu 41, katika shambulio lililodaiwa kufanywa na askari wa IS.
Machi
13:
Watu 37 waliuawa na askari wa Kikurdi katika bomu kurushwa katika gari jijini
Ankara.
Februari 17: Watu 28 walikufan katika shambulio
jijini Ankara.
No comments:
Post a Comment