Amina Athuman (kulia) wakati wa uhai wake alipohudhuria Kongamano la Michezo lililoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) hivi karibuni Mkuza Kibaha katika Kituo cha Michezo cha Filbert Bayi. |
Na Mwandishi Wetu
MWANDISHI wa Habari za michezo wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na
Burudani, Amina Athumani amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali
ya Mnazi Mmoja Zanzibar.
Amina alikuwa visiwani Zanzibar kikazi, kuripoti michuano ya Kombe la
Mapinduzi na Mwenyezi Mungu akamuongoza kuifanya kazi yake vizuri mwanzo hadi
mwisho.
Usiku wa kuamkia safari ya kurejea Dar es Salaam Jumamosi ndipo Amina
aliyekuwa ana uja uzito wa miezi saba alipoanza kusumbuliwa kiafya.Na inaelezwa
asubuhi wakati anaelekea kwenye boti kurejea Dar es Salaam alianguka na
kupelekwa hospitali binafsi, baadaye akahamishiwa Mnazi Mmoja. Siku hiyo hiyo
Amina akajifungua mtoto ambaye kwa bahati mbaya alikwishafariki dunia.
Na usiku wa kuamkia leo naye amefariki pia. Taarifa zaidi za msiba huo zinatarajiwa
baadaye kutoka kwa wahusika, hususan familia ya marehemu na waajiri wake, Uhuru
Publication Limited. Mungu ampumzishe kwa amani Amina Athumani.
Amina wakati wa uhai wake alikuwa ni mmoja wa wadau wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), ambapo alikuwa hakosi katika press au shughuli za kamati ambazo mara nyingi hufanyika Mwananyamala au katika Kituo cha Michezo cha Filbert Bayi Mkuza, Kibaha mkoani Pwani.
Bwana alitoa na Bwana alitwaa, jina lake lihimidiwe. Amina.
No comments:
Post a Comment