WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof.
Makame Mbarawa amesema serikali italipia haraka vifaa vya ujenzi wa jengo la
tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA-TBIII) vilivyokwama bandarini.
Prof. Mbarawa alisema hayo hivi karibuni mara
baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, ambapo alijibu
moja ya changamoto zilizosomwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya
ndege Tanzania (TAA), Salim Msangi kuwa vifaa vya ujenzi vimekwama
bandarini.
“Hivi vifaa vitalipiwa haraka ili mradi uendelee na
kumalizika kwa wakati kama ilivyosemwa utakamilika mwishoni mwa mwezi Desemba
mwaka huu,” alisema Prof. Mbarawa.
Alisema anaamini kukamika kwa jengo hili litakuwa
bora kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, kwa kuwa litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni
sita kwa mwaka, na litapunguza msongamano uliokuwepo katika jengo la pili la
abiria (JNIA-TBII), ambalo lilijengwa kwa ajili ya kuhudumia abiria 1.5 milioni
kwa mwaka, lakini sasa linahudumia abiria 2.5 milioni kwa mwaka.
Awali, Prof. Mbarawa alisema hii ni mara ya tatu
kutembelea jengo hili, na amefanya hivyo ili kumsimamia mkandarasi kwa karibu
aweze kutoa mradi mzuri usiokuwa na tatizo kwa siku za usoni.
Pia alisema serikali imejipanga kuboresha miundombinu
ya viwanja vya ndege ili ndege yake ya Shirika la ndege (ATCL), ambayo
imezindua safari zake katika baadhi ya mikoa iweze kutoa na kupaa bila tatizo.
Mkurugenzi wa Mradi wa Jengo la tatu la abiria
(TBIII), Mhandisi Mohammed Millanga
akitoa maelezo ya kina kwa Waziri, Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza
kushoto), alipotemebelea na kukagua jengo hilo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa TAA, Bw. Salim Msangi.“Huu mradi wa TBIII sio pekee, vipo viwanja 13
vitaboreshwa kwa kufanyiwa ukarabati na upanuzi, na baadhi yake ni Mwanza, JNIA
TBII, KIA, Songwe, Sumbawanga, Tabora, Shinyanga na Kigoma,” alisema Mhe. Prof.
Makame Mbarawa.
Awali akisoma taarifa fupi ya mradi wa TB III, Kaimu
Mkurugenzi, Msangi alisema mradi huo umekumbwa na changamoto ya upatikanaji
wa fedha kiasi cha Euro 121,634,888.30, ambazo serikali kupitia Wizara ya Fedha
na Mipango iliahidi kukamilisha taratibu upatikanaji wa fedha mapema ili kutoathiri
utekelezaji wa mradi.
Pia Msangi alisema changamoto nyingine ni
uchelewaji wa malipo ya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwa vifaa vilivyopo
bandarini hadi sasa inadaiwa Tsh. Bil. 1,362,801,347.00, kati ya fedha hizo
Tsh. Mil. 960,153,258.00 ni za kulipia vifaa maalumu vya usalama vya ukaguzi wa
abiria (X-ray machine), ambavyo vinatakiwa visiathiriwe na joto.
“Hali hii ya vifaa kuchelewa kutoka inasababisha
kuongeza gharama za mradi pamoja na kuchelewesha kazi zilizopangwa kufanyika,
na pia hali hii itasababisha uharibifu wa vifaa ambapo serikali itabidi
kuvilipia pindi itakapotokea uharibifu,” alisema Bw. Msangi.
Hatahivyo, Msangi alisema ujenzi wa jengo hilo utakaotumia
gharama ya Tsh. Bilioni 560, sasa umekamilika kwa asilimia 66.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAHUSIANO CHA TAA
No comments:
Post a Comment