Kocha wa timu ya mpira wa kikapu ya wanawake ya JKT
Stars, Mhoja Nyawawa akizungumza jijini Dar es Salaam leo.
|
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya JKT Stars imetamba kufanya kweli katika
mashindano ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam yatakayofanyika kuanzia
Januari 28 kwenye Uwanja wa Taifa wa Ndani.
Kocha Mkuu wa JKT Stars, Mhoja Nyawawa amesema leo
wakati wa mazoezi ya timu hiyo kuwa, wamejiandaa vizuri na wanatarajia kutwaa
ubingwa huo wa mpira wa kikapu kwa timu za wanawake.
Nyawawa alisema kuwa wachezaji wake wanaendelea
kujifua kwenye uwanja huo wa Taifa wa Ndani na maandalizi yanakwenda vizuri.
Alipoulizwa sababu za timu yake kufanya vibaya katika
mashindano ya Kanda ya Tano yaliyofanyika mwaka jana, kocha huyo alisema kuwa,
hawakupata muda wa kutosha wa maandalizi, lakini sasa wamejiandaa kwa muda
mrefu.
Alisema wachezaji wake walikuwa wametoka likizo siku
chache kabla ya kuanza kwa mashindano yale ya Kanda ya Tano.
Alisema kuwa anajivunia wachezaji wake wenye uzoefu
mkubwa kama akina Ruru Joseph, Evodia Kazinja, Neli Anyengisye, Sekela Dominic,
Angela Agnas na Joyce Kaila.
Alisema haoni timu yenye uwezo wa kuizuia JKT Stars, kwani
timu hiyo imekaa pamoja kwa muda mrefu na bado inaendelea na mazoezi kila siku
kwenye uwanja huo.
No comments:
Post a Comment