Multchoice-Tanzania Wahakikisha shoo ya Diamond inafunika
Jumatano January 11, 2017
ILI kuwapa watanzania wengi uhakika wa kushuhudia michuano ya kombe
Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017,
Kampuni ya Multichoice Tanzania kupitia
king’amuzi chake maarufu cha DStv, itaonyesha michuano hiyo katika kifurushi
chake cha bei ya chini kabisa maarufu kama DStv Bomba. Kifurushi hicho
kinachopatikana kwa bei ya sh 19,975 tu, ni miongoni mwa vifurushi vya
bei nafuu katika huduma ya ving’amuzi hapa nchini.
Akizungumza katika mkutano na waandisha wa habari leo, Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Multichoice Tanzania Salum
Salum, ametanabahisha kuwa kwakuwa DStv ndicho king’amuzi pekee
kitakachoonyesha michuno hiyo mubashara kupitia chaneli yake ya michezo ya
SuperSport4 (DStv 204), wameamua kuiweka michuano hiyo kwenye kifurushi cha bei
nafuu kabisa cha Bomba, ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kuiona michuano
hiyo moja kwa moja.
“Tunajivuna kuwa na sisi Tanzania tumepiga hatua kubwa sana na sasa
hatuna sababu yoyote ya kuona michezo iliyerekodiwa, bali na sisi tunaitazama
mubashara kupitia king’amuzi chetu bora cha DStv, tena kwenye kifurushi nafuu
cha Bomba” alisema Salum na kuongeza kuwa kwa kuwa hii itawapa nafasi
watanzania wengi kufurahia michuano hiyo kila mahali ikiwemo kwenye kumbi za
burudani na hata majumbani.
Wakati huohuo, DStv na Wizara ya Habari Utamaduni Michezo na Sanaa,
imefanikisha safari ya Mwanamuziki wa kizazi kipya hapa nchini Nasibu Abdul
(Diamond) katika kufanikisha onyesho lake katika ufunguzi wa mashindano ya
AFCON nchini Gabon.
Diamond ni miongoni mwa wasanii teule watakaotumbuiza katika hafla hiyo
kitendo ambacho kimechukuliwa na watanzania wengi kuwa ni fursa ya Tanzania
kusikika katika mashindano hayo japokuwa timu yetu haikuweza kufuzu kushiriki.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, utamaduni, michezo na sanaa Nape
Nnauye alisema kuwa kuwepo kwa Diamond kwenye uzinduzi wa michuano hiyo ni
kitendo cha kujivunia na kwamba serikali ikishirikiana na DStv imefanya
jitihada kubwa kufanikisha safari ya WCB kuelekea Gabon.
Kwa upande wake Diamond aliishukuru Serikali na DStv kwa ushirikiano wao
hususan kufanikisha safari yao ya kuelekea Gabon. Aliongeza kuwa jitihada
binafsi za Waziri wa Habari ziliwezesha zoezi hilo kufanikiwa na kwamba
wanaahidi kuwa hawaendi kama WCB, bali kama watanzania na watahakikisha kuwa
wanaipeperusha vema bendera ya Tanzania katika onyesho hilo.
Michuano ya AFCON ya mwaka huu inanogeshwa zaidi na uwepo wa wachezaji
nguli ulimwenguni hususan wale wanaochezea vilabu vikubwa kama Manchester
United, Arsenal, Chelsea, Real Madrid na vilabu vingine vikubwa duniani. Wababe
wa kabumbu kama Mohamed Elneny, Eric Bailly, John Obi Mikel, Pierre Aubemayang,
Riyad Mahrez, Sadio Mane na Victor Moses ni miongoni mwa vigogo watakaoonyesha
umahiri wao katika michuano hiyo.
Mtifuano huo wa AFCON mwaka huu unafanyika katika nchi ndogo ya Gabon,
huku jumla ya timu 16 zikishiriki ikiwemo Uganda ambayo ndiyo timu pekee
iliyofuzu kutoka Afrika Mashariki.
Tayari vuguvugu la michuani hiyo limeshaanza kushika kasi mitaani ambambo
mashabiki wa timu mbalimbali wamekuwa wakitambiana kila mmoja akidai timu yake
itanyakua ubingwa mwaka huu.
Michuona ya AFCON 2017 inadhaminiwa na kampuni ya Total, na itaanza
tarehe 14 January na fainali itakuwa tarehe 05 Februari. Tayari ratiba kamili
ya michuano hiyo imeshatolewa na inapatikana katika tovuti ya www.dstv.com.
No comments:
Post a Comment