*Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wachangia Sh. Milioni 5
Na Mwandishi
Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), hivi karubuni
ilitoa hundi yenye thamani ya Sh. 5,200,000 kwa Tanzania Youth Alliance For
Development and Corporation (TYADCO), kwa ajili ya kupambana na malaria kwa
watoto wenye ulemavu.
Hundi hiyo ilikabidhiwa kwa mwenyekiti wa (TYADCO), Aloyce
Masana na Mwanasheria Mkuu wa TAA, Ramadhani Maleta kwa niaba ya Mkurugenzi
Mkuu wa mamlaka hiyo, Suleiman S. Suleiman.
Akizungumza kwa niaba ya Suleiman, Maleta, ambaye pia ni
wakili alisema kuwa, mamlaka yao inatambua kuwa, malaria ni ugonjwa hatari
ambao hupoteza maisha ya watoto, vijana na hata wazee kwa wingi hapa nchini.
Mwanafunzi wa shule ya sekondari Jangwani akisoma risala wakati wa uzinduzi wa kongamano hilo. |
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo ni jukumu letu sote
kushirikiana katika kuhakikisha kuwa tunapambana na hatimaye kuutokomeza kabisa
ugonjwa huu, ambao ni tishio hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitatu
na mama wajawazito.
Suleiman alisema kuwa kamwe Watanzania tusikubali ndoto
za vijana wetu hawa za kuwa Marubani,
Waandisi, Wanasheria, Waandishi wa Habari n.k zisipotee kwa kukatishwa na vifo
vinavyotokana na ugonjwa wa malaria.
Wanafunzi wakicheza mchezo wa kuigiza wakati wa uzinduzi wa kongamano hilo. |
“Nadhani
wakati umefika sasa kwa kila mmoja wetu kuhakikisha anashiriki kikamilifu
katika mapambano haya ya kuutokomeza ugonjwa huu, kwani kila vita hii sio ya
watu au taasisi fulani, Hii ni vita ya wote na ndio maan sisi TAA hatukusita
kushiriki kongamano hili la kuchangia, “alisema.
Uzinduzi huo ulikwenda sambamba na kongamano maaluma la
kuzuia malaria kwa watoto wenye ulemavu, ambapo zaidi ya watoto 300
walihudhuria kutoka shule na taasisi mbalimbali zilishiriki katika ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Pia katika kongamano hilo kulijadiliwa masuala ya haki za
wanafunzi na watoto wenye ulemavu, afya kwa vijana, pamoja na elimu ya
kujitambua kwa wote.
TAA kama zilivyo taasisi zingine za kiserikali hapa nchini,
inatilia mkazo sana umuhimu wa haki za watoto wenye ulemavu, afya na elimu ya
ufundi stadi kwa watoto hao.
Suleiman alisema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha
tunawasaidia vijana hao kwa ujumla ili waweze kukabiliana na changamoto
mbalimbali za kijamii pamoja na kufikia malengo ya Millenia.
Mbali na TAA kuchangia kiasi cha Sh. Milioni 5, Kampuni ya
Mabibo Beer Wine & Spirits kupitia kwa Mama Rugemalila, ilitoa kiasi cha
Sh. Milioni 3 kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao walemavu kupambana na malaria.
Naye Masana alisema kuwa, kongamano hilo lilihusu pia
kujadili mapungufu yaliyopo baina ya matumizi ya pombe, madawa ya kulevya na
mimba za utotoni, ambavyo huwagusa pia vijana wenye ulemavu.
Kingine ni kutathimini na kutoa mpango mkakati wa kupambana
na tatizo la kukata tamaa kwa watoto wenye ulemavu.
Aidha, shule ya sekondari ya Jangwani ilisema kuwa pamoja na
ukongwe wao, lakini bado wanafuzi wao walemavu wanapata shida ya usafiri, hivyo
waliomba wasaidiwe gari.
Baadhi ya wanafunzi waliohudhuria uzinduzi wa kongamano la kupiga vita malaria kwa watoto wenye ulemavu lililofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni. |
Naye Rugemalira alisema kuwa kampuni yao kama kampuni
zingine za kijamii hapa nchini inatilia mkazo sana umuhimu wa elimu na afya kwa
watoto wenye ulemavu na hivyo adhma yao ni kuangalia jinsi ya kuwasaidia watoto
hao ili waweze kufikia malengo yao.
Pia, aliyaomba mashirika mbalimbali, taasisi za kidini na
zingine kuwa bega kwa bega katika kusaidia watoto wenye ulemavu kukabiliana na
changamoto zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment