Thursday 2 April 2015

Mwanariadha atishiwa kifo baada ya kutoa siri za ubakaji za kocha



LONDON, England
MMOJA kati ya wanariadha mahiri katika mbio ndefu duniani na mshirika wa Mo Farah katika mazoezi amekuwa akiishi kwa wasiwasi mkubwa nchini Uganda, baada ya kutishiwa kifo kufuatia kutoa madai kuwa kocha wake alikuwa akiwanyanyasa kijinsia wanariadha wakike, wengine wenye umri wa miaka 15.

Moses Kipsiro (pichani), ambaye alifanikiwa kutetea taji lake la Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 10,000 huko Glasgow, Scotland mwaka jana, alisema wiki hii kuwa, baadhi ya wakimbiaji wakike walikwenda kwake wakitaka msaada.

Alisema kuwa mara kwa mara amekuwa akipokea vitisho vya kuuawa baada ya kuwasilisha madai hayo ya wanariadha wakike kwa Shirikisho la Riadha la Uganda na polisi.

Jumatatu Kipsiro aliwasilisha kwa polisi vitisho hivyo kupitia ujumbe mfupi wa maneno jijini Kampala, Uganda.

Mwanariadha huyo alisema kuwa anataka kuondoka Uganda yeye na mke wake na watoto watatu endapo polisi watashindwa kuchunguza madai yake. Wanatakiwa wailinde familia yangu, alisema.

Habari hiyo kwa mara ya kwanza ilipelekwa katika gazeti la Sportsmail na Pace Sports Management, ambao pia wanamuwakilisha bingwa mara mbili wa Olimpiki Farah.

Akizungumza wiki hii, mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 28 Kipsiro alisema mwaka jana alifuatwa na wanariadha watano wakike katika kambi ya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya kushiriki mashindano ya mbio za nyika za Afrika.

Kipsiro anasema kuwa walikwenda kwake kama mwanariadha mkongwe, mtu mzima na nahodha wa timu ya taifa na anayeshikilia rekodi ya taifa na alishinda medali katika kiwango cha dunia na ana medali tatu za Jumuiya ya Madola, ambapo walilalamika kuwa, kocha amekuwa akiwabaka wanariadha hao.

Moses Kipsiro amekuwa akifanya mazoezi na Mo Farah.
Kwa mujibu wa wasichana hao kocha huyo aliwaambia kuwa anataka awatie mimba na baadae kuzitoa, kwa sababu kwa kufanya hivyo kunapanua sehemu zao nyeti na kuwawezesha kukimbia kama Wakenya, aliniambia Kipsiro.

Nilikwenda katika Shirikisho la Riadha na polisi. Lakini hadi sasa hakuna chochote kilichofanyika. Mbali na kupata vitisho vya kifo, kaka yangu naye pia alitishiwa na kukamatwa.

Na hadi sasa nimetemwa katika timu ya taifa ya Uganda. Na sijakimbia katika mbio za dunia za nyika huko China wikiendi iliyopita kwa sababu yah ii tu.

Viongozi wa Shirikisho la Riadha la Uganda walipinga madai hayo lakini taarifa ya kina ilitoka katika gazeti la Uganda, ambalo lilifanya mahojiano na wanariadha watatu wakike ambao walikuwa kambi kwa miezi mitatu huko Kapchorwa Machi mwaka jana.

 Alikuja katikati ya siku na katika chumba chetu, alisema mwanariadha mmoja aliyezungumza na Daily Monitor.

Alitishia kututimua kambini endapo tungetoa siri au kumuangusha. Kambini hakukuwa na kocha mwanamke, hivyo hatukuwa na pakukimbilia…. 
Katika makala hiyo hiyo nahodha Kipsiro alikaririwa.
Nilikorofishana naye lakini matokeo yake ndio hayo, alisema. Nilichogundua kilichowahusisha wanawake ni cha kushangaza sana, kilinishtua sana,’ alisema na kuongeza:

‘Siku moja aliwakusanya wakimbiaji wa timu ya wasichana ya vijana katika maeneo ya siri na kuwaambia ili kukimbia vizuri lazima wafanye ngono au kuzaa. Nadharia yake ilikuwa hivi endapo sehemu za siri za mwanamke zitapanuka , miguu yake itakwenda haraka. Nilishtushwa kusikia upuuzi huo… 
.
`Bahati mbaya baadhi ya watu wanaamini kuwa ni kocha mzuri. Hadi sasa wanaendelea kumtetea.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha la Uganda (UAF) Beatrice Ayikoru alikaririwa katikahabari hiyo hiyo akikanusha madai hayo.

 Madai yote dhidi ya kocha ni ya uongo, alisema. Nilikutana na wanariadha huko Kampala na hakuna hata mmoja aliyezungumzia jambo hilo.

Kwa mujibu wa Pace Sports Management, ambao wana mkataba na UAF wakizungumzia suala hilo wiki hii, madai hayo yanachunguzwa na viongozi pamoja na polisi lakini bado matokeo ya uchunguzi hayajatolewa.

No comments:

Post a Comment