Kikosi cha Yanga. |
Na Seba Nyanga
HAKUNA wa kuizuia Yanga leo kutwaa ubingwa wa
Tanzania Bara kwa mara ya 25 wakati itakapocheza na Polisi Morogoro katika
mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa leo tunaweza kuufananisha na ule
usemi wa sungura kumkaba tembo, kwani Yanga katika ligi hiyo ni sawa na tembo
wakati Polisi Moro inafananishwa na sungura kutokana na uwezo na udogo wake.
Kwa sababu ya kutokuwepo wa kuizuia Yanga
ndio maana tayari wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hiyo wameandaa
sherehe na kutoa ratiba kamili ya kusheherekea ubingwa huo.
Kimsimamo; Yanga ambayo ni bingwa wa
kihistoria wa Tanzania na iliyopo kileleni ikiwa na pointi 52, inahitaji pointi
tatu tu ili iweze kuwa bingwa kamili wa msimu wa 2014/15 na kujikatia tiketi ya
kuliwakilisha taifa katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Ikiifunga Polisi Moro leo itakuwa imefikisha
jumla ya pointi 55, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kati ya 13
zinazoshiriki ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.
Azam inayoshika nafasi ya pili ikiwa na
pointi 45 inaweza kufikisha pointi 54 tu tena endapo itafanikiwa kushinda mechi
zake zote zilizobaki.
Ni kweli katika soka lolote linaweza kutokea,
lakini ukilinganisha uwezo wa Yanga, hivyo leo kama Polisi Moro itaifunga timu
hiyo yenye maskani yake katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, basi ni
sawa na mende kuangusha kabati, kitu ambacho ni ngumu kutokea.
Katika mchezo wao wa kwanza, Yanga iliibamiza
Polisi Moro kwa mabao 5-0 katika mzunguko wa kwanza, hivyo ni dhahiri kuwa timu
hiyo haina ubavu kuzuia makali ya Yanga.
Taarifa za Yanga zilisema kuwa uongozi wa
klabu hiyo tayari umeanza maandalizi kusherehekea ubingwa kwa mtindo wa aina yake.
“Uongozi wa Yanga unapenda kuwaalika wanachi wa Tanzania na nchi jirani
kuungana nasi leo Jumatatu katika shamra shamra za ushindi wa ubingwa wa
michuano ya Ligi Kuu,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
“Sisi kama Yanga tumejipanga kwa staili ya tofauti kabisa
katika kuuchukua ubingwa wa Ligi Kuu,” iliongeza taarifa hiyo.
Naye kocha Hans van der Pluijm alisema
anatarajia timu yake kutwaa ubingwa leo.
Yanga watasafiri kwenye Tunisia kucheza mechi
ya marudiano ya Kombe la Shirikisho na Etoile de Sahel ya huko itakayochezwa
mwishoni mwa wiki hii.
No comments:
Post a Comment