Mwanariadha Alphonce Simbu akimaliza mbio za Mumbai Marathon. |
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison
Mwakyembe kesho atakuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuiaga timu ya taifa ya riadha itakayoshiriki mashindano ya 166 ya Dunia yatakayofanyika jijini London, Uingereza kuanzia Agosti 4 hadi 13.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mawasiliano wa DStv, Johson
Mshana, Mwakyembe atakabidhi bendera hiyo kwa timu hiyo katika hafla
itakayofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Timu hiyo ambayo iko chini ya Kocha Mkuu, Zakaria
Barie ina wachezaji nane, ambao ni Alphonce Simbu, Stephano Huche na Said Makula
ambao watakimbia marathon wakati Gabrie Geay na Emmanuel Giniki watashiriki
mbio za meta 5,000 huku Sara Ramadhani na Magdalena Shauri watashiriki marathon
kwa upande wa wanawake na Failuna Abdi atashiriki meta 10,000.
Wengine watakaokuweo katika timu hiyo itakayoondoka
nchini keshokutwa Jumanne ni pamoja na Francis John, ambaye ni kocha msaidizi wa timu hiyo.
Barie akizungumza kutoka Arusha jana kwa njia ya simu
alisema kuwa timu hiyo imejiandaa vizuri na iko tayari kupambana kwa ajili ya
kupata medali kutoka katika mashindano hayo, ambayo kwa mara ya mwisho Tanzania
ilipata medali mwaka 2005 kutoka kwa Christopher Isegwe aliyepata medali ya
fedha katika maratoni mashindano hayo yalipofanyikia Helsinki, Finland.
Kocha huyo alisema kuwa timu yake haina majeruhi
wowote na inaondoka ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika
mashindano hayo makubwa kabisa ya riadha duniani.
Alphonce Simbu (kushoto) akiwaongoza wenzake katika mazoezi ya timu ya taifa ya riadha itakayoshiriki mashindano ya dunia baadae mwezi huu. |
Naye Simbu alisema kuwa wamejipanga kurudi na medali
licha ya ugumu uliopo mbele yao, kwani wanajua ushindani mkali uliopo mbele yao.
Hafla hiyo imedhaminiwa na DStv, na tayari Katibu
Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday aliondoka jana kwenda London
kuhudhuria vikao vitakavyofanyika mapema kabla ya kuanza kwa mashindano hayo
akimwakilisha rais wake, Anthony Mtaka.
Aidha, mashindano ya mwaka huu yatakuwa ya aina yake
kwani wanariadha bora wawili duniani, Usain Bolt wa Jamaica na Mo Farah wa
Uingereza watastaafu rasmi mbio baada ya kushirikiria ubingwa wa dunia kwa
muda mrefu,
Hizo zitakuwa mbio za mwisho kwa Bolt katika
mashindano ya dunia na Farah naye hatakimbia tena mbio za meta 5,000 na 10,000
au mbio za uwanjani na badala yake atageukia marathon, ambazo ni mbio za
kilometa 42.
No comments:
Post a Comment